Afisa
Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) Bibi
Nasama Massinda akiwasilisha mada leo Mjini Dodoma kwa Wabunge wa
Kamati ya Bunge ya Biashara, Viwanda na Mazingira na Kamati ya Bunge ya
Uwekezaji( hawapo pichani)kuhusu uanzishwaji wa Masoko ya Bidhaa hapa
nchini ili kuwainua wakulima.
Mkurugenzi
wa Usimamizi na Uendelezaji wa Masoko Kutoka Mamlaka ya Masoko ya
Mitaji na Dhamana Bw. Godfrey Malekano akijibu hoja za Wabunge (hawapo
pichani) kuhusu hatua zinazochukuliwa katika kuwasaidia wakulima kupitia
Masoko ya Bidhaa ili waweze kunufaika na bidhaa wanazozalisha.
Mbunge
wa Newala Mjini Mhe. George Mkuchika akichangia mada juu ya namna bora
ya kuwainua wakulima hapa nchini hasa wanaozalisha Korosho na mazao
mengine ya biashara wakati wa semina kuhusu Masoko ya Mitaji na Dhamana
iliyofanyika Mjini Dodoma leo.
Baadhi
ya Wabunge wakifuatilia mada kuhusu Masoko ya Bidhaa iliyowasilishwa
wakati wa Semina ya kuwajengea uwezo Wabunge wa Kamati ya Biashara
Viwanda na Mazingira na Kamati ya Bunge ya Uwekezaji kuhusu mikakati ya
mamlaka hiyo kuwainua wakulima hapa nchini.
Mkurugenzi
wa Bodi ya Korosho Tanzania Bw. Mfaume Juma akijibu hoja za Wabunge
kuhusu mikakati ya Bodi hiyo kuimarisha zao la korosho ili liweze
kuwainua wananchi kiuchumi wakati wa semina kuhusu Masoko ya Mitaji na
Dhamana iliyofanyika Mjini Dodoma leo.
(Picha Zote Na: Frank Mvungi – MAELEZO – Dodoma)
…………………………………………………………………………………………………………….
Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Kilimo kinachangia asilimia 26 ya
pato la Taifa na kuchangia zaidi ya asilimia 75 ya kipato kwa wananchi
waishio vijijijini, pamoja na mchango mkubwa wa kilimo kwenye uchumi wa
nchi, wakulima wamekuwa wakipata matatizo mbalimbali ya masoko yenye bei
zenye ushindani.
Kwa kuliona hilo Serikali
ilipitisha sera ya masoko ya bidhaa mwaka 2014 kwa kuanza na mazao manne
ya majaribio ambayo ni, Korosho, Ufuta, Alizeti na Mchele.
Hayo yamesemwa leo, mjini Dodoma
na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA)
Bibi. Nasama Massinda wakati wa semina kwa Wabunge juu ya uanzishwaji
wa masoko ya bidhaa nchini iliyoandaliwa na mamlaka hiyo.
Akieleza kazi kuu za soko la
bidhaa Massinda amesema kuwa soko la bidhaa linaleta uwazi wa bei za
mazao na mwenendo wa soko, kila mtu ataweza kujua bei ya mazao sokoni
ambapo bei zitatolewa kwa vyombo vya habari pamoja na kuondoa ulazima wa
wakulima kusafirisha mazao yao toka eneo moja kwenda lingine kutafuta
wanunuzi.
“Vile vile soko la bidhaa
litasaidia kutoa bei zenye ushindani kwa kuzingatia upatikanaji wa
bidhaa na mahitaji ya bidhaa, litaboresha bei ya mazao vijijini kwa kuwa
na soko la bidhaa litakalo toa taarifa kwa wakulima wote kuhusu soko,
bei na mwenendo wa soko,” alifafanua Massinda.
Kwa upande wake Mbunge wa
Nanyamba, Mhe. Abdallah Chikota alilitaka soko hilo kupanua wigo wa
uelimishaji kwa kushuka mpaka kwa wakulima na watendaji wa Serikali
katika ngazi ya chini kuliko kuishia kwa mawakala ambao wanaweza wasitoe
elimu hiyo kama ilivyotarajiwa.
Soko hilo la Bidhaa linalotarajia
kuanza Septemba mwaka huu linategemea kumnufaisha mkulima mdogo,
wakulima wakubwa, wenye viwanda, wakusanya mazao (ushirika), wauzaji
mazao nje, wakopeshaji na vyombo vya fedha pamoja na Serikali kupata
mapato kupitia tozo kutokana na uwepo wa takwimu na uwazi.
0 maoni:
Chapisha Maoni