WAKAZI
wa Kijiji cha Nditu,
Kata ya Suma, Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, wamegoma kuzika mwili wa marehemu Shabani Yusufu (27),
baada kushambuliwa na kundi la
siafu nyumbani kwake na
kusababisha apoteze uhai.
Yusufu, amefariki dunia ikiwa ni siku
moja tu baada ya kufunga ndoa na kuzua gumzo kubwa kijijini hapo.
Alikutwa na mauti hayo akiwa
amejipumzisha ndani usiku wa kuamkia jana, jambo ambalo linahusishwa na imani
za kishirikina.
Akisimulia mkasa huo, baba mzazi wa
marehemu, Ebron Mwaipaja, alisema mwanawe
alitoka kufunga ndoa juzi na
alikutwa na mauti hayo akiwa amejipumzisha chini ya mti nyumbani kwake, ambako
ghafla alivamiwa na siafu.
Alisema kulikuwa na maneno ya hapa na
pale wakati wa maandalizi ya harusi hiyo kutoka kwa baadhi ya watu, ambayo
yamesababisha tukio hilo kuhusishwa na imani za kishirikina.
Baba huyo alisema baada ya tukio hilo,
wananchi na uongozi wa Serikali ya kijiji walifika eneo hilo, huku wakimtaja
mmoja wa wanakijiji kuwa ndiye “aliyetuma” siafu hao.
“Wananchi waligoma kuandaa taratibu za
mazishi wakishinikiza aletwe mganga wa jadi apige ramli ili kumbaini mtu
anayeendesha matukio ya ushirikina yanayoendelea kijijini hapa,” alisema.
Alisema baada ya wananchi kugoma kuzika,
Serikali ya kijiji nayo iligoma kutoa kibali, ikisema siku zote Serikali
haiamini uchawi, jambo ambalo lilisababisha wananchi waliokujwa na silaha za
jadi, kufanya maandamano na kufunga barabara.
Baada ya hali ya usalama kuzidi kuwa
mbaya, polisi walifika eneo la tukio na kutuliza ghasia, huku familia ikifanya
maandlizi ya maziko bila wanakijiji kuhusika.
“Kijana wangu ndiyo kwanza alitoka
kufunga ndoa akifurahia maisha ya kuwa na mke, amekutwa na umauti tena kwa
kuvamiwa na siafu wakati kijiji hiki hakijawahi kuwa na wadudu hawa, yote
namwachia Mungu,” alisema Mwaipaja.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake,
Joseph Kajura, alisema wanafahamu fika tukio hilo ni la kishirikina na ndiyo
maana walimtafuta mganga wa kienyeji ili apige ramli kwa ajili ya kubaini
mhusika.
Na Kalulunga Blog
0 maoni:
Chapisha Maoni