—————————-
Waganga wa tiba asili ambao
wamekuwa wakitoa huduma ya tiba pasipo kujisajili wametakiwa kujisajili
Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala ili waweze kutambulika kisheria.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Hamis Kigwangalla ameyasema hayo
leo, Bungeni Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge
Viti Maalum Mhe. Zainabu Mussa Bakar juu ya udanganyifu unaofanywa na
waganga wa tiba asili wa kutoa dawa feki kwa wagonjwa.
“Waganga wa tiba asili wapo
kisheria, ni kweli wapo wanaotoa dawa feki, na wengi wao ni wale ambao
hawajasajiliwa, hivyo tumewaagiza kujisajili ili tuweze kuwatumbua na
dawa zao ziweze kuhakikiwa na kusajiliwa kwa ajili ya matumizi ya
binadamu,” alifanunua Mhe. Kigwangalla.
Mhe. Kigwangalla amesema kuwa,
mganga yoyote atakaye kiuka agizo hilo la kujisajili basi hatua kali
zitachukuliwa dhidi yake. Aidha, amesema Wizara iko makini na
ufuatiliaji wa dawa feki nchini kwani wanapopata fununu ya uwepo wa dawa
feki hutuma kikosi kuchunguza na ikibainika kuwa dawa ni feki basi
hatua kali huchukuliwa kwa muhusika.
Aliendelea kwa kusema kuwa, ili
kudhibiti uingizwaji wa dawa feki nchini Wizara hiyo hufanya uhakiki wa
muda mrefu kuchunguza iwapo dawa inayopendekeza kuingia nchini siyo feki
na inafaa kwa matumizi ya binadamu, ikiwa dawa haina madhara yoyote
basi inasajiliwa kwa ajili ya kuingia sokoni.
Vilevile Mhe. Kigwangalla amesema
kuwa, Wizara imewaagiza waganga wa tiba asili kufunga dawa zao kwa
kutumia vifungashio maalum vya madawa ambavyo vitasaidia dawa hizo
kuendelea kuwa salama kwa mtumiaji kwa kipindi kilichopangwa kutumika.
0 maoni:
Chapisha Maoni