Alhamisi, 30 Juni 2016

Bodaboda waiomba serikali kuwachukulia hatua kali abiria wanaokataa kuvaa helmeti

bodaBodaJonas Kamaleki, Maelezo
——————————
WAAENDESHA pikipiki maarufu kama bodaboda wameiomba serikali kuwachukulia hatua kali abiria wanaokataa kuvaa kofia ngumu (Helmet) ili kutoa fundisho kwa watu wengine wasihatarishe maisha yao.
Akiongea katika mahojiano maalum, mwendesha pikipiki, Nathanael Kiula wa Dar es Salaam amesema kuwa abiria wanaokataa kuvaa helmeti wachukuliwe hatua kali ikiwepo kutozwa faini isiopungua Tsh. 30,000/=  ili liwe fundisho kwa wengine.
“Mimi nina helmeti mbili ya kwangu na abiria lakini abiria wengi hawataki kuvaa helmeti hasa akina mama kwa madai kuwa nywele zao zinaharibika pia wanadai kuwa zina uchafu.”alisema Kiula.
Kiula alisema kuwa elimu itolewe kwa abiria na waendesha pikipiki juu ya umuhimu wa kuvaa helmeti kwani ni kwa manufaa yao wanapopata ajali wasiumie sana au kupoteza maisha na si kwa ajili ya kuwakwepa matrafiki.
Mwendesha pikipiki aliyejitambulisha kwa jina la Isaac William alisema abiria wanaokataa kuvaa helmeti waadhibiwe vikali ili kukomesha tabia hii isiokubalika katika suala zima la usafirishaji.
“Abiria wangu baadhi wanakubali kuvaa helmeti lakini walio wengi hukataa kuzivaa kwa madai kuwa wanaogopa magonjwa ya kuambukizwa kupitia vifaa hivyo,”alisema William.
Naye abiria wa bodaboda ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam, Bi Fatuma Abdallah amesema yeye hawezi kuvaa helmeti kwani zinatumiwa na watu wengi hivyo anaogopa kupatwa na magonjwa.
“Siwezi kuvaa mikofia yao kwani inatumiwa na watu wengi huwezijua wana magonjwa ya ngozi kiasi gani, kamwe sintoyavaa ng’o,”alisema Fatuma.
Kwa upande wake Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchi, Mohamed Mpinga alisema kuwa uvaaji wa kofia ngumu kwa waendesha pikipiki ni lazima. Anayekaidi amri hiyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Helmet Vaccine Initiative Tanzania Foundation, Bw. Alpherio  Nchimbi alisema matumizi ya Helmeti hayaepukiki kwa usalama wa mwendesha pikipiki na abiria.
“Kwa umuhimu huo, Taasisi yetu inatoa msaada wa kiufundi kwa Jeshi la Magereza nchini kwa ajili ya uanzishwaji wa kiwanda cha kutengeneza kofia ngumu kwa kufuata viwango vya Shirika la Viwango nchini (TBS) na pia tunatoa elimu kwa bodaboda kuhusu matumizi ya kofia ngumu na madhara yatokanayo na kutovaa kofia hizo kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa kwa ujumla,” alisema Nchimbi.
Kuhusu suala la kuvaa helmeti, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema kuwa mwendesha pikipiki na abiria ni lazima wavae helmeti na ifikapo Julai 1, 2016 hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya abiria au mwendesha pikipiki atakayekaidi amri hiyo.
“Nawaambia, hatutamvumilia mtu yeyote, mwendesha pikipiki na abiria asiyevaa helmeti tunawahesabu kuwa wana mpango wa kujiua,”alisema Makonda wakati wa Uzinduzi wa Mpango wa Taifa wa Usalama wa raia wa Jeshi la Polisi.
Suala la kuvaa kofia ngumu au helmeti kwa waendesha pikipiki na biria wao limekuwa likipuuzwa kwa muda mrefu ndio maana serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na Jeshi la polisi wameandaa utaratibu wa kuwafuatilia na kuwachukulia hatua za kisheria kwa ajili ya kunusuru maisha yao. Mpango huu unaanza rasmi tarehe 1, 2016.

0 maoni:

Chapisha Maoni