Kaimu
Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri akizungumza
wakati wa kufunga mkutano wa Wachumi na Maafisa Mipango uliofanyika
katika ukumbi wa Hazina, Dodoma.
………………………………………………………………………………………………
Na Joyce Mkinga
SEKTA Binafsi katika ngazi zote ni
lazima ishirikishwa katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo
2016/17 – 2020/21 uliozinduliwa hivi karibuni.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya
Mipango Bibi Florence Mwanri aliyasema hayo alipokuwa akifunga mkutano
wa Wachumi na Maafisa Mipango uliofanyika mjini Dodoma mwishoni mwa
wiki.
Bibi Florence Mwanri amesema sekta
binafsi ni wadau muhimu katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa
Maendeleo hivyo, wanatakiwa kushirikishwa katika mipango yote ya
Serikali.
“Katika mipango yetu katika ngazi
zote lazima sekta binafsi ishirikishwe kwa sababu wao ndio watekelezaji
wakubwa wa mpango huo” alisema Bibi Mwanri
Amesema maafisa mipango wanapoibu
miradi mbalimbali katika ngazi ya kijiji, wilaya, mkoa ni lazima sekta
binafsi ishirikishwe ili kuwapa fursa nzuri ya kushiriki kikamilifu
katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo ambao unalenga katika
Kujenga Uchumi wa Viwanda ili Kuchochea Mageuzi ya Kiuchumi na
Maendeleo ya watu
Mkutano huo uliwashirikisha
wachumi na maafisa mipango 170 kutoka katika wizara, idara za serikali,
sekretarieti na mikoa na wilaya, taasisi za utafiti, na sekta binafsi
ulikuwa na kaulimbiu ya Kuelekea kwenye Utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo 2016/17 – 2020/21.
Lengo kuu la Mkutano huo ilikuwa
ni kujenga uelewa wa pamoja juu ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka
Mitano na utelekezaji wake.
Mpango huo unatarajia kugharimu Trilioni 107 ambapo Sekta binafsi itachangia Trilioni 48.
Akiwasilisha maazimio ya mkutano
huo Kaimu Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango kutoka Klasta ya
Uchumi Jumla, Dkt. Lorah Madete amesema Serikali na sekta binafsi
wakutane pamoja na kupanga mikakati ya kutekeleza mpango huo wa
maendeleo.
Vile vile, Dkt Madete alisema kuwa
kuna haja ya Serikali kuingiza Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia
katika mipango ya Serikali ikiwa ni pamoja na Mpango wa Taifa wa
Maendeleo wa Miaka Mitano.
Mkutano huo uliandaliawa Tume ya Mipango kwa ushirikiano na Taasisi ya Uongozi.
0 maoni:
Chapisha Maoni