Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akihutubia kwenye uzinduzi wa kituo cha Mawasiliano cha Polisi Call
Centre Biafra Kinondoni.
…………………………………………………………………………………………………
Jonas Kamaleki, MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amelitaka jeshi la polisi
nchini kuwadhibiti majambazi ipasavyo kwa kuwanyanganya silaha kwenye
matukio ya kiuharifu ili kukomesha vitendo viovu katika Taifa.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Usalama wa Jamii.
“Inashangaza jambazi anavamia
kituo cha polisi anaua na anaondoka wakati polisi wapo na wana silaha na
risasi wanazo lakini wanashindwa kumnyang’anya silaha,”alishangaa Rais
Magufuli.
Ameongeza kuwa ujambazi na
vitendo vya uharifu nchini inabidi vikomeshwe mara moja ili watanzania
waishi kwa amani na kufanya maendeleo kwani wananchi wanataka maendeleo.
Akiongelea kuhusu maslahi na
vitendea kazi kwa jeshi la polisi, Rais Magufuli amesema kuwa serikali
yake itafanya kila iwezalo kuliwezesha jeshi hilo ili liweze kufanya
kazi kwa ubora zaidi.
Rais Magufuli ameonyesha kuwa na
imani na jeshi la polisi licha ya kuwa na kasoro ndogo ndogo kwa baadhi
ya polisi ambao wanalichafua jeshi hilo.
Aidha ametoa agizo kwa TCRA kushirikiana na jeshi la polisi nchini ili kuweza kurekodi simu na kutoa print out mara moja tofauti na ilivyo sasa.
Kuhusu kundi la wafanyakazi
wanaofanyakazi kwenye Dawati la Taarifa la polisi, Mhe. Rais amemtaka
Mkuu wa Jeshi hilo, IGP Ernest Mangu kuwafikiria na kuwapatia posho ya
kazi kwani kazi wanayoifanya ni ngumu mno na inahitaji umakini zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam, Paul Makonda amemwomba Mhe. Rais kuliongezea fedha jeshi
hilo ili liweze kufanya kazi kwa ustadi zaidi na kukomesha vitendo vya
uharifu nchini.
Makonda amelipongeza jeshi la polisi kwa kudhibiti matukio ya ujambazi hapa nchini hususan kwenye mabenki.
Mpango huu wa Usalama wa Jamii
umezinduliwa leo na utadumu hadi 2019 na unatarajiwa kutoa matokeo
makubwa ya kudhibiti uharifu nchini.
0 maoni:
Chapisha Maoni