Mwenyekiti
waTimu ya Bunge (Bunge Sports Club) Mhe. William Ngeleja akizungumza na
waandishi wa habari kuhusu mechi kati ya wabunge ambao ni wapenzi wa
timu ya Simba na wapenzi wa timu ya Yanga itakayofanyika mwezi Agosti
2016 kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutatua tatizo
la madawati hapa nchini kwa kuhamasisha wadau kuchangia madawati
yatakayo gawanywa katika Halmashauri zote nchini.
…………………………………………………………………………………………………………..
Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania wameandaa mechi maalum kwa ajili ya kuchangia
madawati shule za msingi na sekondari, ili kuunga mkono Serikali ya
awamu ya Tano kutatua kero ya upungufu wa madawati Nchini.
Mwenyekiti wa Timu ya Bunge
(Bunge Sports Club) Mhe. William Ngeleja ameyasema hayo leo Mjini Dodoma
katika mkutano na waandishi wa habari alipokuwa akiitambulisha kamati
itakayoratibu mchezo huo.
Aidha mechi kama hizo zimekuwa
zikiandaliwa kila baada ya kuahirishwa kwa Bunge na kuhusisha mpira wa
miguu kati ya wabunge ambao ni wanachama na wapenzi wa timu ya Simba kwa
upande mmoja na wale wa Yanga kwa upande mwingine.
“Mashindano yatakayofanyika mwaka
huu ni kwa ajili ya kupata madawati mengi kadri itakavyowezekana kutoka
kwa wadau mbalimbali ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya
Tano kutatua kero ya upungufu wa madawati shule za msingi na sekondari
nchini,” alifafanua Mhe. Ngeleja.
Mhe. Mgeleja aliendelea kusema
kuwa, ili kufanikisha mashindano hayo uongozi wa timu ya Bunge (Bunge
Sports Club) umeunda kamati maalum ya maandalizi ili kufikia lengo
lililokusudiwa kwa kuwatembelea na kuwahamasisha wadau mbalimbali Nchini
Ili wachangie madawati.
Wabunge waliochaguliwa katika
kamati hiyo ni Mwenyekiti Mhe. John Peter Kadutu (Ulyankulu), Makamu
Mwenyekiti Mhe. Mussa Azzan Zungu (Ilala) pamoja na wajumbe Mhe. Salim
Hassan Turky (Mpendae), Mhe. Ridhiwani Kikwete (Chalinze), Mhe. Mwigulu
Nchemba (Iramba Magharibi), Mhe. Dkt. Dalaly Kafumu (Igunga).
Wajumbe wengine ni Mhe. Raphael
Chegeni (Busega), Mhe. Mansoor Hiran (Kwimba), Mhe. Ahmed Shabiby
(Gairo), Mhe. Bonna Kaluwa (Segerea), Mhe. Zaynab Vulu (Viti Maalum),
Mhe. Abdul-Aziz Abood (Morogoro Mjini) na Mhe. Venance Mwamoto (Kilolo).
Aidha Mhe. Ngeleje amesema kwamba
ameitambulisha kamati hiyo ili wadau waweze kuwatambua na kusiwe na
maswali mara wajumbe hao wanapokutana na wadau kwa ajili ya kuwaomba
kuchangia madawati au fedha zitakazonunulia madawati na baadaye
kukabidhiwa Serikalini ili yaweze kusambazwa Nchi nzima.
Vile vile amewaomba wadau ambao
wako tayari kushirikiana na wabunge katika uchangiaji wa madawati basi
wasisite kuonana na kamati hiyo na kutoa michango yao.
Waratibu na waandaaji wa
mashindano hayo ni Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na uongozi wa (Bunge
Sports Club) ambapo mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa Ogasti 15, 2016
0 maoni:
Chapisha Maoni