Kikosi cha Yanga. |
WACHEZAJI wa zamani wa Yanga na Simba wameitaka Yanga kutobweteka
katika mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe na
badala yake watulie na kutumia vyema uwanja wa nyumbani kupata matokeo
mazuri.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, wachezaji hao
walisema Yanga ilionesha kandanda nzuri katika mchezo dhidi ya Mo Bejaia
isipokuwa safu ya ushambuliaji haikucheza kwa utulivu.
Miongoni mwa wachezaji hao ni Mwanamtwa Kihwelu na Moses Mkandawile
waliosema kuwa Yanga inaweza kupata matokeo mazuri iwapo kama
hawatabweteka, na ikiwa watapambana kwa ushirikiano.
Kihwelu alisema: “TP Mazembe sio timu nyepesi kwani ina uzoefu wa
mashindano hayo, na tayari wana pointi tatu na kuhimiza Yanga kutulia
kwenye uwanja wa nyumbani kutengeneza nafasi zenye kuzaa matunda.”
Alisema kinachohitajika ni mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara
kuzidisha mara mbili kiwango chao ili kuwa na uhakika wa kuibuka na
ushindi. Kihwelu alipendekeza kuwa iwapo Juma Abdul na mchezaji mpya
Obrey Chirwa watakuwepo kuna uwezekano wa kupata ushindi mzuri.
Kwa upande wake, Mkandawile aliwahimiza Yanga kucheza wakijua kuwa
wako kwenye uwanja wa nyumbani. Alisema ni muhimu kuzingatia nidhamu kwa
ajili ya kuepukana na kadi nyingi zisizokuwa na tija .
Golikipa huyo wa zamani wa Simba alisema sehemu inayohitaji kufanyiwa
kazi ni safu ya ulinzi na ushambuliaji, kwani wanahitaji kucheza kwa
utulivu mkubwa. Yanga wanatarajiwa kushuka dimbani Juni 28, mwaka huu
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa pili hatua ya
makundi. Kwa sasa wanaendelea kujifua na mazoezi katika kambi yao
iliyoko nje ya nchi Uturuki na kesho wanatarajiwa kurudi.
0 maoni:
Chapisha Maoni