—————————————————
Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Viwanda vilivyobinafsishwa na Serikali ambavyo haviendelezwi kutwaliwa ili kutolewa kwa wawekezaji wenye uwezo wa kuviendesha.
Waziri wa Viwanda, Biashara na
Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage ameyasema hayo leo mjini Dodoma alipokuwa
akijibu swali la Mbunge wa Tabora Mjini Mhe. Emmanuel Mwakasaka
aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa juu ya mwekezaji wa kiwanda cha
nyuzi Tabora kwa kushindwa kuendeleza kiwanda hicho.
“Wizara kwa kushirikiana na Ofisi
ya Msajili wa Hazina inaendelea na tathmini ya viwanda vyote
vilivyobinafsishwa na Serikali kikiwemo kiwanda cha nyuzi cha Tabora ili
kujiridhisha kama wawekezaji wa viwanda hivyo wanatimiza matakwa ya
mkataba na Serikali,” alifafanua Mhe. Mwijage.
Aliendelea kwa kusema kuwa, ikiwa
viwanda hivyo vitabainika kubadilishwa matumizi yake au kutoendelezwa
basi Serikali itavirudisha kwa watanzani ili viweze kuendelezwa.
Aidha Mhe. Mwijage amesema kuwa,
kwa sasa mwitikio wa kuviendeleza viwanda ambavyo vilikuwa havizalishi
ni mzuri kwani viwanda vingi vimeanza kufanya kazi lakini kwa wale ambao
watashindwa kabisa kuviendeleza basi viwanda hivyo vitarejeshwa kwa
watanzania.
Vile vile Mhe. Mwijage amesema
kuwa dhana ya Serikali ya awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa viwanda
inaenda pamoja na kurejesha Serikalini viwanda vyote vilivyobinafsishwa
lakini haviendelezwi ili vitolewe kwa wawekezaji wengine.
Sambamba na hayo Mhe. Mwijage
amesema kuwa kufufua viwanda, hasa viwanda vya nguo ni pamoja na
wakulima wa pamba kulima zao hilo kwa wingi kwa ajili ya uchakataji
pamoja na kudhoofisha uingizaji wa nguo za mitumba nchini.
Wizara hiyo inaendelea na
kushawishi wawekezaji mbalimbali ili kujenga viwanda vingi iwezekavyo
kwa ajili ya uchakataji wa mazao yanayolimwa nchini pamoja na mifugo.
0 maoni:
Chapisha Maoni