Timu
ya Taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’
imeondoka saa 9.45 alfajiri ya leo Juni 30, 2016 kwa ndege ya Shirika la
Ndege la Ethiopia kwenda Visiwa va Hame-Shelisheli kwa ajili ya kuwavaa
wenyeji katika mchezo wa marudiano kuwania nafasi ya kufuzu fainali za
Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana.
Serengeti
Boys inaondoka na matumaini makubwa ya kuiondoa Shelisheli katika mbio
hizo baada ya kuvuna ushindi mnono wa mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza
uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Jumapili ya Juni 26, 2016.
Ili ifuzu, Serengeti Boys inahitaji kusimama imara katika matokeo hayo
ama kwa kupata sare ya aina yoyote, kushinda au ikitokea kupoteza, basi
isifungwe zaidi ya mabao 2-0.
Lakini
Kocha Mkuu wa vijana hao, Bakari Shime maarufu kama Mchawi Mweusi
kutoka Tanga, amesema, “Nawaheshimu Shelisheli, lakini vijana wangu
hawawezi kuwapa nafasi hata kidogo wapinzani wetu. Hapa tulishinda, na
kwako tunakokwenda tunakwenda kushinda. Vijana wangu wa Serengeti Boys
wako vizuri. Nawapenda na wao wanatupenda makocha wao na viongozi wote
wa TFF.”
Katika
mchezo wa Dar es Salaam waliozifumania nyavu walikuwa Nickson Kibabage,
Ibrahim Abdallah na Ally Hussein ambaye alifunga ambao kila mmoja
amepania kufunga kama kocha akiwapa nafasi ya kuanza katika kikosi cha
kwanza kwa sababu Mchawi Mweusi amefunga safari hiyo akiwa na kikosi cha
nyota 20 wa timu hiyo inayolelewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) chini ya Rais Jamal Malinzi.
Nyota
waliosafiri ni pamoja na makipa, Ramadhani Awm Kabwili na Samwel Edward
Brazio wakati mabeki wako Kibwana Ally Shomari, Nickson Clement
Kibabage, Israel Patrick Mwenda, Dickson Nickson Job, Ally Hussein
Msengi, Issa Abdi Makamba.
Viungo
ni Kelvin Nashon Naftal, Ally Hamisi Ng’anzi, Asadi Ali Juma Ali,
Syprian Benedictor Mtesigwa, Ibrahim Abdallah Ali, Yassin Muhidini
Mohamed, Shaban Zuberi Ada huku washambuliaji wakiwa ni Rashid Mohammed
Chambo, Mohammed Abdallah Rashid, Yohana Oscar Mkomola, Muhsin Malima
Makame na Enrick Vitalis Nkosi.
Serengeti
Boys ambayo haina mdhamini badala yake ikihudumiwa na TFF yenyewe
ilikuwa kambini tangu Juni 14, 2016 kujiandaa na mechi hizo za kufuzu
fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Shelisheli na Afrika
Kusini ambayo itapambana nayo baadaye mwezi ujao.
Katika
kuajindaa na mchezo huo, Serengeti Boys ilifanya ziara India ambako
walishiriki mashindano ya vijana ya Kimataifa yanayotambuliwa na FIFA
(AIFF International Youth Tournament 2016) kabla ya kurudi na rekodi ya
kupigiwa mfano si tu katika Tanzania na kwa nchi za Afrika Mashariki.
Ilishika nafasi ya tutu nyuma ya Korea Kusini na Marekani.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA SOKA TANZANIA
0 maoni:
Chapisha Maoni