PELUM TANZANIA YATOA MAFUNZO YA HAKI ZA ARDHI MKOANI IRINGA
WAJUMBE wa kamati za uamuzi za vijiji 10
vya wilaya za kilolo na Mufindi mkoani Iringa wamepata mafunzo ya haki za ardhi
na utawala yatakayowaongezea uelewa juu ya sheria za ardhi, haki za ardhi kwa
wanawake na makundi maalum pamoja na utatuzi wa migogoro ya ardhi.
Mafunzo hayo yaliyofanywa kwa siku nne
katika kila wilaya yametolewa na mtandao wa Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali
yanayofanya kazi na wakulima na wafugaji wadogo nchini Tanzania (PELUM
Tanzania).
Afisa Mradi wa PELUM Tanzania, Angolile
Rayson alivitaja vijiji hivyo kuwa ni pamoja na Ikuka, Mbigili, Mawala,
Mawambala na Masalali kwa upande wa wilaya ya Kilolo na Isaula,
Magunguli, Makungu, Usokami na Ugesa kwa upande wa wilaya ya Mufindi.
Alisema mafunzo hayo yanatolewa kupitia
mradi wa kuhusisha jamii ya vijijini katika uwajibikaji wa masuala ya ardhi ya
kijiji unaojulikana kwa jina la CEGO unaotekelezwa kwa uratibu wa mtandao huo
na ufadhili kutoka shirika la kimataifa la maendeleo la Marekani (USAID).
Rayson alisema mradi huo wa miaka minne
ulianza kutekelezwa mwaka 2013 ukihusisha pia vijiji vingine 20 vya wilaya nne
katika mikoa ya Morogro na Dodoma.
“Shughuli kuu za mradi huo ni kuongeza na
kuimarisha uelewa wa haki za ardhi kwa wananchi wa vijijini pamoja na viongozi
wao kupitia mafunzo, machapisho na mijadala mbalimbali,” alisema.
Alisema lengo likiwa ni kuhakikisha
kunakuwepo na matumizi mazuri na endelevu ya ardhi ya kijiji kwa ajili ya
uhakika wa chakula na kipato kwa wananchi.
Akifunga mafunzo hayo wilayani Mufindi
juzi, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Isaya Mbenje alisema
ardhi ni mojawapo ya rasimilali muhimu sana kwa maendeleo ya kijamii na
kiuchumi katika nchi.
“Hivyo ni muhimu kwa jamii yetu kuwa na
uelewa wa kutosha juu ya sera na sheria za ardhi ili ardhi ya Tanzania itumike
kwa manufaa ya watanzania wote na kwa usawa,” alisema.
Akiishukuru PELUM Tanzania kwa kuleta
mradi huo mkoani Iringa, Mbenje ili matumizi yake yawe endelevu ni muhimu
wananchi vijijini wakaijua Sheria ya ardhi namba 4 na 5 ya mwaka 1999.
“Na ni muhimu uelewa wa viongozi juu ya
majukumu yao katika usimamizi wa ardhi ya kijiji, na utatuzi wa migogoro ya
ardhi kwa njia ya amani pasipo kuvunja mahusiano mazuri baina ya watumiaji wa
ardhi ukaongezeka,” alisema.
Awali mmoja wawashiriki wa mafunzo hayo,
Festo Katingasa wa kijiji cha Usokami, Mufindi alisema mafunzo ya matumizi bora
ya ardhi waliyopata kupitia mradi huo atayatumia kusaidia utatuzi wa migogoro
ya ardhi katika kijiji chake.
“Chanzo cha migogoro mingi ya ardhi
katika kijiji chetu ni ukosefu wa hati miliki za ardhi inayoonesha mipaka aya
ardhi kwa matumizi mbalimbali,” alisema.
Naye Salima Nyato wa kijiji cha Magunguli
alisema kwa miaka mingi wanawake wamekuwa wakikosa haki ya kumiliki ardhi na
kwamba mafunzo hayo yatawasaidia kuipata haki hiyo.
0 maoni:
Chapisha Maoni