Jumatatu, 27 Juni 2016

TAMKO KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI,

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
TZTAMKO KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI, PAMOJA NA MLIPUKO WA UGONJWA WILAYANI CHEMBA NA KONDOA, MKOANI DODOMA,  LILILOTOLEWA NA MHE. UMMY MWALIMU (MB); WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, TAREHE 27 JUNI, 2016
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto inaendelea na utaratibu wa kutoa tahadhari kwa wananchi na maelekezo ya hatua za kuchukua katika kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu. Huu ni mwendelezo wa utoaji wa taarifa ya kila wiki, kuhusu mwenendo wa ugonjwa huu kama tulivyoahidi. Hadi kufikia tarehe 26 Juni 2016, jumla ya wagonjwa 22,185 wametolewa taarifa, na kati yao, watu wapatao 344 wamepoteza maisha, tangu ugonjwa huu uliporipotiwa mnamo mwezi Agosti 2015.
Takwimu zinaonyesha kuwa, katika wiki hii inayoishia   tarehe 26 Juni 2016, idadi ya wagonjwa wa Kipindupindu walioripotiwa ni 365 na hakuna aliyepoteza maisha.  Idadi kubwa ya wagonjwa hawa walitolewa taarifa kutoka wilaya ya Ukerewe (316) ambapo imejumlisha wagonjwa kutoka tarehe 7 Aprili hadi tarehe 21 Juni 2016. Hivyo, wagonjwa wa Kipindupindu wapya walioumwa kati ya 20 hadi 26 Juni 2016 pekee ni takriban 49. Takwimu hii inaashiria kuwa wagonjwa wameongezeka kidogo ikilinganishwa na wiki iliyotangulia, ambapo kulikuwa na wagonjwa 46 na vifo viwili. Mikoa iliyoripoti ugonjwa wa Kipindupindu wiki hii ni Morogoro (Morogoro mjini 15, Kilosa 9 na Mvomero 3), Mara (Tarime vijijini 18), Mwanza (Ukerewe 319) na Arusha (Arusha Vijijini (1).

0 maoni:

Chapisha Maoni