Na Daudi Manongi,MAELEZO
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu
amewataka wakuu wa wilaya na mikoa kuhakikisha wanamaliza zoezi la
upatikanaji wa madawati kwa shule za msingi na sekondari.
Mhe. Suluhu ameyasema hayo leo
Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati wakuu wa wilaya na mikoa walipokuwa
Ikulu wakila kiapo cha maadili ya viongozi kabla ya kwenda kuapishwa na
wakuu wa mikoa yao.
Aidha amewaagiza viongozi hao
kusoma alama za nyakati kwa kuangalia makosa ya waliokuwepo kabla yao
ili kuhakikisha hawarudii makosa yaleyale.
Mhe.Suluhu pia amesema kuwa
Serikali haitaki kusikia wananchi wanalia njaa na hivyo wakuu wa wilaya
wahakikishe chakula kinapatikana katika maeneo yao kwani hilo ni jukumu
lao.
Aliongeza kuwa wakuu wa wilaya
wana majukumu makubwa ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma zote za
muhimu katika maeneo yao kwani wananchi wana mategemeo makubwa juu yao.
Aidha ameagiza wakuu wa Wilaya
hao kufanya kazi karibu na Maafisa Tarafa ili kujua kero za wananchi na
kuzifanyia kazi kwa kasi ili wananchi wafaidike na maendeleo yawafikie
kwa haraka.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene
ivi karibuni aliwaagiza wakua wa wilaya na mikoa kuhakikisha wanatimiza
agizo la Rais John Pombe Magufuli kuhakikisha hakuna mwanafunzi
atakayekaa chini kwa uhaba wa madawati kufikia June 30,2016.
0 maoni:
Chapisha Maoni