Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akizungumza kwenye kikao
na mabalozi kutoka Ujerumani na Denmark (hawapo pichani) hivi karibuni
katika Ukumbi wa Wizara jijini Dar es Salaam.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo(Katikati) akiwa katika
picha ya pamoja na Balozi wa Ujerumani, Egon Kochanke(Kulia) na Balozi
wa Denmark, Einar Jensen(Kushoto).
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo(Kulia) akijadiliana
jambo na Balozi wa Denmark, Einar Jensen (Kushoto). Katikati ni Balozi
wa Ujerumani, Egon Kochanke akiweka sahihi kwenye kitabu cha wageni
ofisini kwa Waziri jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
…………………………………………………………………………………………
- Kina thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.5
- Kuzalisha tani milioni 1.35 kwa mwaka
Na Devota Myombe
Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo amekutana na Balozi wa Ujerumani nchini
Tanzania, Egon Kochanke pamoja na Balozi wa Denmark nchini, Einar Jensen
kujadili ujenzi wa Kiwanda cha mbolea wilayani Kilwa.
Katika mkutano huo, ilielezwa
kuwa matayarisho ya ujenzi wa kiwanda hicho cha mbolea chenye thamani ya
Dola za Marekani bilioni 1.5 yanaendelea na kwamba kiwanda hicho
kinatarajiwa kuzalisha tani milioni 1.35 za mbolea kwa mwaka.
Waziri Muhongo alisema ardhi kwa
ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho ipo na kuwa gesi asilia itakayotumika
kiwandani hapo ipo ya kutosha.
Alisema kampuni mbalimbali kutoka
ndani na nje ya nchi zitakuwa na hisa katika kiwanda hicho ambapo kwa
upande wa Tanzania, alizitaja kampuni hizo kuwa ni Shirika la Maendeleo
ya Petroli Tanzania (TPDC), Minjingu Mines pamoja na Shirika la Taifa la
Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Aidha, kwa upande wa kampuni za
nje, Profesa Muhongo alizitaja kuwa ni Ferrostaal ya Ujerumani, Haldor
Topsoe ya Denmark na Fauji kutoka nchini Pakistan.
Profesa Muhongo aliwahakikishia
mabalozi hao pamoja na ujumbe wao kuwa ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa
kiwanda hicho ipo na kwamba gesi asilia itakayohitajika ipo ya kutosha
na kuwa bado nafasi za uwekezaji zinapatikana. “Ardhi ipo, gesi ipo
hivyo mnakaribishwa,” alisema Prof. Muhongo.
Naye Balozi wa Ujerumani nchini,
Egon Kochanke alimshukuru Profesa Muhongo kwa kukubali kukutana na
ujumbe huo kupokea maombi ya mpango wa ujenzi wa Kiwanda hicho cha
mbolea ambapo alisema, hiyo ni njia mojawapo ya kuboresha uzalishaji
Tanzania. “Nimefurahi sana kushiriki kikao hiki na nina kushukuru kwa
kukubali kwako kupokea maombi haya,” alisema.
Kwa upande wake Balozi Einar
Jensen alitumia nafasi hiyo kumshukuru Profesa Muhongo kwa jinsi
alivyoupokea ujumbe huo na namna alivyoendesha majadiliano husika.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na baadhi ya watendaji wa Wizara pamoja na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini.
0 maoni:
Chapisha Maoni