Mnamo tarehe 19 Juni 2016, Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wanawake, Wazee na watoto ilitoa taarifa kuhusu kuwepo kwa Ugonjwa usiofahamika katika Wilaya za Chemba na Kondoa, Mkoani Dodoma. Kwa wakati huo kulikuwa na jumla ya wagonjwa 21 na vifo 7. Leo napenda kuchukua nafasi hii kutoa taarifa ya hali ya ugonjwa.
Mpaka kufikia tarehe 24 Juni 2016, idadi ya wagonjwa imefikia 32, na idadi ya vifo imebakia 7. Hii ni baada ya kuongezeka kwa wagonjwa 11 katika kipindi cha wiki moja. Aidha, tangu ugonjwa huu ujitokeze jumla ya wagonjwa 12 (vifo 3) wamepatiwa huduma katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, na 18 (vifo 4) wametibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kondoa. Wagonjwa 2 hawakuwahi kulazwa hospitali.
Hadi jana kulikuwa na jumla ya wagonjwa 9 ambao wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa ya Dodoma, na 14 wako katika Hospitali ya Wilaya ya Kondoa. Wagonjwa watatu waliolazwa Hospitali ya Mkoa Dodoma, na wawili waliolazwa Kondoa, bado hali zao ni tete.
Katika jitihada za kutambua kiini cha ugonjwa huu, Wizara imepeleka jopo la Wataalam huko Dodoma ili waweze kushirikiana na wenzao walioko huko kufanya uchunguzi wa kina wa ugonjwa huu. Aidha, sampuli mbalimbali zikiwemo damu, haja ndogo, haja kubwa, vinyama vya ini, na sampuli za vyakula zilipelekwa katika maabara za Mkemia Mkuu wa Serikali, Maabara ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Maabara ya Taifa ya Magonjwa ya Binadamu na Maabara ya Hospitali ya KCMC (KCRI).
Vile vile sampuli nyingine zimepelekwa nchini Marekani katika maabara ya Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa cha Marekani (CDC) jijini Atlanta kwa ajili ya uchunguzi zaidi. Hadi sasa, ni sampuli za nafaka pekee, zilizofanyiwa uchunguzi katika Maabara ya TFDA ndio zilizoonyesha kuwepo kwa uchafuzi wa sumukuvu (Aflatoxin) katika sampuli za nafaka hizo,
kama ifuatavyo; Jumla ya sampuli 13 kati ya 27 (48%) zilikuwa na uchafuzi wa sumukuvu (aflatoxins) kwa kiasi kisichokubalika kwenye nafaka kwa mujibu wa viwango vya kitaifa na zote zilitokana na mahindi; Kati ya sampuli hizo zenye sumukuvu, 12 zilitoka wilaya ya Chemba na sampuli 1 ilitoka wilaya ya Kondoa.
Sampuli saba (7) kati ya hizo 12 zilikuwa na kiasi kikubwa cha sumukuvu kinachozidi 150 µg/kg (micrograms per kllogram) kwa total aflatoxins, ambapo wigo wa aflatoxin B1 katika sampuli hizo ni kati ya 157.1 – 194.4 µg/kg.
Kiasi kama hicho kiliwahi kuhusishwa na madhara yatokanayo na sumukuvu (aflatoxins) katika nchi za India, China na Kenya. Dalili za madhara ya sumukuvu (aflatoxins) zinafanana na dalili za ugonjwa usiofahamika uliojitokeza katika Wilaya za Chemba na Kondoa
Hivyo upo uwezekano mkubwa kwamba ugonjwa huu umesababishwa na ulaji wa chakula kilichokuwa na sumukuvu na kuleta madhara. Ili kuwa na uhakika wa jambo hili Wizara yangu inasubiri matokeo ya vipimo vya damu na haja ndogo vilivyopelekwa kwa uchunguzi zaidi katika Maabara ya CDC, Atlanta iliyopo nchini Marekani. Matarajio yetu ni kupata majibu hayo katika kipindi kisichozidi wiki moja.
Ndugu waandishi wa Habari, kufuatia matokeo hayo napenda kusisitiza mambo yafuatayo; Kwanza kabisa, nasisitiza kuwa haya bado ni matokeo ya awali miongoni mwa uchunguzi unaofanywa katika kubaini kwa uhakika chanzo cha ugonjwa huu, lakini ni vyema tukaanza kufanyia kazi matokeo haya wakati tukiendelea kusibiri uchunguzi unaoendelea kufanyika katika maabara nyingine nje ya Nchi.
Wizara yangu itaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na TAMISEMI katika kipindi hiki cha kutambua na kudhibiti ugonjwa huu.
Tutashirikiana na mamlaka husika za kitaifa, kimkoa na kiwilaya ili kuhakikisha kuwa nafaka ambazo zina sumukuvu kwa kiasi kisichokubalika hazitumiwi kwa chakula; Tunaendelea kutoa Elimu kwa wananchi juu ya njia sahihi za uandaaji wa chakula utakaosaidia kupunguza kiasi cha sumukuvu (aflatoxin) kwa nafaka ambazo hazijaharibika sana. Njia hizi ni pamoja na kuchambua nafaka zilizoharibika (zilizooza, kuvunjika, zilizobadilika rangi),
kukoboa mahindi kabla ya kusaga au kuacha kutumia nafaka zitakazoonekana kuharibika sana; Serikali itaendelea kuimarisha mikakati ya kitaifa ya kupunguza uchafuzi wa sumukuvu katika vyakula, ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo wa kupima sumukuvu katika damu na mkojo miongoni mwa taasisi za ndani ya nchi Tutaendelea kutoa matibabu kwa wanachi walioathirika na Ugonjwa huu, kwenye Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na Hospitali ya Wilaya ya Kondoa.
Tutaendelea kushirikiana na mashirika ya kimataifa kama WHO na CDC katika kudhibiti ugonjwa huu.
Ndugu Waandishi wa Habari, Wizara itaendelea kutoa taarifa za mara kwa mara kwa wananchi kuhusu ugonjwa huu kadri taarifa muhimu zitakavyokuwa zikipatikana. Aidha, ninatoa rai kwa jamii, kuendelea kushirikiana na wataalamu wanaoshughulika na ugonjwa huu, na pale atakapopatikana mgonjwa basi apelekwe haraka katika kituo cha Afya cha karibu, ili aweze kusaidiwa.
Natoa shukurani kwa makundi ya jamii, watu na mashirika ya Kimataifa, na wadau wengine wote, kwa mchango wao mkubwa katika jitihada zetu za kuutambua na kudhibiti ugonjwa huu.
KUHUSU UTARATIBU WA UTOAJI CHAKULA HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI
Wiki iliyopita Hospitali ya Taifa Muhimbili, ilitoa utaratibu mpya wa huduma ya chakula kwa wagonjwa ambapo kila mgonjwa alitakiwa atoe sh.6000/= ili apate chakula kwa siku nzima
Hii ni moja ya juhudi kubwa zinazofanywa na Uongozi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili katika kuboresha huduma kwa wagonjwa ikiwemo kuboresha upatikanaji wa dawa na chakula.
Hata hivyo, nimepokea maoni mengi kutoka kwa Wananchi na Wadau mbalimbali kuhusiana na hatua iliyochukuliwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambapo itaanzisha utaratibu utakaowezesha wagonjwa kuchangia gharama ya chakula ili chakula kiweze kuandaliwa na Hospitali badala ya utaratibu wa sasa ambapo mgonjwa huletewa chakula kutoka kwa ndugu wanaomhudumia.
Kufuatia hali hii kuleta wasiwasi kwa wananchi na wagonjwa, nimeagiza Hospitali ya Taifa Muhimbili kusitisha utaratibu huo mpaka hapo tutakapopata taarifa za kutosha kuhusu faida na hasara za utaratibu mpya unaopendekezwa.
Imetolewa na:-  
Ummy Mwalimu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto