Mwanasheria
Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju akijibu hoja za Wabunge mapema leo
Bungeni Mjini Dodoma wakati akihitimisha hoja kuhusu muswaada wa sheria
ya marekebisho ya sheria mbalimbali wamwaka 2016.
———————————————-
Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Bunge la Jamhuri wa Muungano wa
Tanzania leo, Mjini Dodoma limepitisha muswada wa marekebisho ya sheria
ya Elimu kifungu kinachoeleza kuwa mtu anayempatia ujauzito mwanafunzi
wa shule ya msingi au sekondari kuwa adhabu yake ni faini isiyozidi
shilingi laki tano au kifungo kisichozidi miaka mitatu.
“Muswada unapendekeza kuwa kifungu
hicho kifutwe na badala yake kitungwe kifungu kipya cha 60A ili kuweka
masharti yanayojitosheleza kuhusu zuio la kuoa au kumpatia ujauzito
mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari, kinapendekeza adhabu yake
iwe kifungo cha miaka 30 gerezani,” alifafanua Mwanasheria Mkuu wa
Serikali Mhe. George Masaju.
Vile vile mtu atakayebainika
kusaidia, kushawishi au kuacha mwanafunzi wa shule ya msingi au
sekondari kuolewa au kuoa anatenda kosa la jinai ambalo adhabu yake ni
faini isiyopungua shilingi milioni tano au kifungo cha miaka mitano
gerezani au vyote kwa pamoja.
Mhe. Masaju aliendelea kwa
kufafanua kuwa, sheria hiyo imependekeza kuwa pale ambapo kosa hilo
litafanywa na mtoto basi adhabu yake itakuwa kwa mujibu wa masharti ya
sheria ya mtoto. Hii ni kwa sababu sheria ya mtoto inakataza mtoto
anayetiwa hatiani kufungwa gerezani.
Aidha marekebisho hayo katika
sheria ya Elimu yanalenga kumjengea mwanafunzi wa shule ya msingi au
sekondari mazingira mazuri ya kumaliza ipasavyo elimu yake kwa ngazi
hiyo.Hivyo basi kila Mkuu wa shule au Mwalimu Mkuu atawasilisha kwa
Kamishna wa Elimu taarifa ya robo mwaka kuhusu matukio ya ndoa na mimba
kwa wanafunzi katika shule yake na hatua zilizochukuliwa.
Sheria ya Elimu inamruhusu
mwanafunzi aliyepewa ujauzito kuendelea na masomo mara tu anapojifungua.
Sheria hiyo inasubiri kuwekwa saini na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli ili ianze kutumika.
0 maoni:
Chapisha Maoni