KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Mkoani Singida imeshindwa kununua, kusafirisha na kuzikabidhi bati 56 zilizokuwa zikabidhiwe katika Kijiji cha Msiu,kata ya Mwanga kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya Kijiji hicho.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi kwa zaidi ya miezi miwili sasa umebaini kwamba mfuko wa jimbo la Iramba mashariki ulitenga jumla ya shilingi milioni mbili kwa ajili ya kununua bati na jengo la zahanati ya Kijiji cha Msiu.
Aidha uchunguzi huo ulibaini pia kwamba zahanati ya Kijiji hicho ilitakiwa kupata mgao wa bati 80,lakini hata hivyo mei,14,mwaka huu uongozi wa Halmashauri hiyo ulikabidhi bati 24 za geji 28 na kuahidi kukabidhi bati 56 zilizobakia mapema iwezekanavyo.
Hata hivyo habari za uhakika zilizopatikana kutoka kwa wananchi wa Kijiji hicho na kuthibitishwa na watendaji wa maeneo hayo zinaeleza kuwa pamoja na jitihada za kufuatilia bati hizo zilizotolewa na mfuko huo wa jimbo wilayani,lakini wamekuwa wakipigwa danadana na afisa mipango wa wilaya hiyo.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka kata ya Mwanga,afisa mtedaji wa kata hiyo,Waziri Husseini Waziri alisema tangu walipopokea bati 24,mei,14,mwaka huu hadi jana juni,24,mwaka huu walikuwa bado hawajapokea akiba ya bati zilizobakia.
Aidha Waziri aliweka bayana kwamba mapema mei,14,wakati afisa mipango wa Halmashauri hiyo,aliyemtaja kwa jina moja tu la Mwinuka akikabidhi bati hizo walifuatana na mbunge wa jimbo la Iramba mashariki,Allani Kiullah na kumuahidi kuwa bati 56 zingekabidhiwa haraka sana ili ujenzi wa zahanati hiyo uweze kukamilika.
“Kutokana na kukabidhi bati 24 kwa uongozi wa Kijiji hicho kunamaanisha kwamba shilingi milioni mbili zilizotengwa kwa ajili ya bati 80 zitakuwa zimenunua bati 24 tu,kitendo hicho kitakuwa ni sawa na kuwaibia wananchi”alisisitiza Waziri
Hata hivyo kwa mujibu wa afisa mtendaji huyo kutotekelezwa kwa ahadi iliyotolewa na afisa mipango wa wilaya hiyo kwa mbunge wa jimbo hilo,kunamaanisha kwamba uongozi wa Halmashauri hiyo ulimdangaanya hata mbunge wa jimbo hilo,Allani Kiullah.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Nduguti,yalipo makao makuu ya wilaya hiyo juu ya tuhuma hizo,Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo,James Mkwega alibainisha kuwa anashangazwa kusikia kutopelekwa kwa bati hizo 56 za zahanati ya Kijiji cha Msiu,kwani walishamuagiza muhusika afanye haraka kuzifikisha ili ziweze kuezekwa kwenye jengo hilo.
“Unaulizia suala la bati za zahanati ya Kijiji cha Msiu,kwani bado hazijapelekwa,mbona tulishaagiza katika kikao cha kamati ya kugawa fedha za mfuko wa jimbo kilichofanyika juni,18,mwaka huu bati hizo zipelekwe haraka Kijijini”alihoji mwenyekiti huyo kwa mshangao sana.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mkalama,Bravo Lyapembile alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo,bila kutoa sababu za kuchelewa kununuliwa na kupelekwa kwa bati hizo alikiri kwamba bati hizo hazijapelekwa na kwmaba jana ijumaa ndiyo zilikuwa zinunuliwe na kupelekwa.
“Bati zenyewe leo ndo zinanunuliwa hazijaletwa zitapokelewa mchanani kweli ntakagua na kubaini ukweli niko nao kikaoni finance”alisisitiza kwa majibu ya ujumbe mfupi Mkurugenzi mtendaji huyo.
Naye mmoja wa wajumbe wa kamati ya mfuko wa jimbo, Habiba Hamisi Omari alishangazwa na taarifa ya kutopelekwa kwa bati hizo mpaka siku ya ijumaa wakati walishaagiza bati hizo zipelekwe haraka ili wananchi wa Kijiji cha Msiu waweze kuendelea na utaratibu wa upauaji wa jengo hilo.
Mwenyekiti wa mfuko huo ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Iramba mashariki,Allani Kiullah akizungumzia mgao huo wa bati alisema anachofahamu yeye ni kwamba bati hizo zilipaswa kuwa zimepelekwa muda mrefu kwa sababu fedha za kununulia zilikwishatengwa muda mrefu na hata kwenye kikao kingine cha kamati hiyo kilichokutana juni,18,walimuagiza afisa mipango kutekeleza makubaliano ya kikao.
DSCN0006
Mabati hayo yakishushwa  na kukabidhiwa kwa uongozi wa Kijiji hicho.
DSCN0008Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Msiu wakionekana kubeba bati kutoka kwenye gari la Halmashauri lililoleta Kijijini hapa
DSCN0014Afisa mipango wa Halmashauri ya wilaya ya Mkalama,Bwana Mwinuka(wa kwanza kutoka kulia) akiwa katika mkutano wa kukabidhi bati 24 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Msiu,wilayanai Mkalalma.(
DSCN0044Mbunge wa jimbo la Iramba mashariki,Bwana Allani Kiullah(wa nne kutoka kushoto) akimkabidhi Mwenyekiti wa Kijiji cha Msiu bati 24 tu zilizonunuliwa na Halmashauri ya wilaya ya Mkalama
Picha zote Na Jumbe Ismailly)