Kocha
Mkuu wa timu ya soka ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ya
Shelisheli, Gavan Jeanne ameonesha kuihofia Serengeti Boys ya Tanzania
katika mchezo wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa
utakaofanyika Juni 26, 2016 kuanzia saa 10.00 jioni kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Jeanne
alionesha hofu hiyo leo Juni 25, 2016 alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari na mbele ya Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Bakari
Shime ambao kwa pamoja walikuwa wakmizungumzia namna walivyoandaa timu
zao kwa ajili ya mchezo huo wa kesho.
“Hatujawahi
kushiriki michuano ya vijana. Hii ni mara yetu ya kwanza. Tumekuja
kujifunza kwa wenzetu Tanzania ambao wana uzoefu,” alisema Jeanne ambaye
pia alithibitisha kuwa hawajawahi kucheza mchezo wa kirafiki wa
kimataifa.
Kwa
upande wa Bakari Shime wa Serengeti Boys, alisema ameindaa mechi hiyo
vema kiakili na kimwili kwa ajili ya kuikabili Shelisheli katika mchezo
huo ambao hamasa yake imekuwa kubwa kwa kuwa kikosi hicho kinaandaliwa
kuwa timu ya taifa baada ya miaka miwili.
Wachezaji
wa Serengeti Boys wamesema, watafanya vema kwenye mchezo huo. Wachezaji
hao ni Anthony Shilole ambaye alisema: “Tumejifunza mambo mengi,
ushindi ni lazima kwa sababu tutafuata maelekezo ya walimu wetu.
Tutajitahidi tushinde.”
Ally Ng’anzi: Maandalizi ni mazuri. Mechi ya Jumapili tumejiandaa vema. Tunashinda tena kwa magoli mengi.”
Ally Msengi: “Watanzania watarajie ushindi baada ya maandalizi ya muda mrefu. Timu iko kambini kitambo.”
Kennedy Nashony: Tutapambana kadiri ya uwezo. Kila mechi kwetu ni fainali. Hatuko tayari kupoteza ili kukosa mechi zijazo.”
Shelisheli
ilitua Ijumaa usiku saa 7.45 usiku ikiwa na viongozi 25 na imefikia
hoteli ya Southern Sun iliyoko katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Waamuzi
wanne kutoka Ethiopia, ndio watakaochezesha mchezo huo. Waamuzi hao ni
Belay Tadesse Asserese ambaye ni mwamuzi wa kati wakati wasaidizi wake
ni Tigle Gizaw Belachew upande wa kulia na Kinfe Yilma Kinfe upande wa
kushoto huku mwamuzi wa akiba atakuwa Lemma Nigussie. Kamishna wa mchezo
huo atakuwa ni Bester Kalombo.
Serengeti
Boys ilikuwa kambini tangu Juni 14, 2016 kujiandaa na mchezo huo wa
kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya vijana wenzao wa
Shelisheli utakaofanyika Juni 26, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa,
jijini Dar es Salaam. Mchezo wa marudiano kati ya Serengeti Boys na
Shelisheli utachezwa Julai 2, 2016 huko Shelisheli.
Katika
kuajindaa na mchezo huo, Serengeti Boys ilifanya ziara India ambako
walishiriki mashindano ya vijana ya Kimataifa yanayotambuliwa na FIFA
(AIFF International Youth Tournament 2016) kabla ya kurudi na rekodi ya
kupigiwa mfano si tu katika Tanzania na kwa nchi za Afrika Mashariki.
0 maoni:
Chapisha Maoni