JESHI
la Polisi Kikosi cha viwanja vya ndege, Dar es Salaam linamshikilia
raia wa Nigeria, Bede Eke (45) kwa tuhuma za kusafirisha unga
unaosadikiwa kuwa ni dawa za kulevya.
Akizungumza
na gazeti hili, Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege Tanzania, Kamishna
Msaidizi wa Polisi, Martin Otieno alisema mtu huyo alikamatwa usiku wa
kuamkia jana akiwa safarini kwenda Lagos, Nigeria.
“Juni
26, mwaka huu majira ya saa 7:25 usiku katika eneo la ukaguzi wa
mashine ya chini, askari Polisi kwa ushirikiano na askari wa uwanja wa
ndege Terminal II walifanikiwa kumkamata Bede Eke akiwa na begi
walilolitilia shaka na katika upekuzi walibaini kuwa na unga,”alisema
Otieno.
Kamanda
Otieno alisema Eke alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere (JNIA) akisafiri kwa Ndege ya Ethiopian Airline kwenda Lagos,
Nigeria kupitia Ethiopia, ambapo baada ya kutiliwa shaka katika begi
hilo waliamriwa kulifungua na ndani palikuwa na begi dogo la mgongoni,
ambalo lilishonwa vizuri na kufungwa na gundi ya nailoni.
Alisema
ndani ya begi hilo dogo la mgongoni jeusi, mlikuwa na kifurushi chenye
uzito wa kilo tano na kilipofunguliwa palikuwa na unga unaodhaniwa kuwa
ni dawa za kulevya.
“Tumepeleka
sampuli ya unga huo kwa mkemia mkuu wa serikali ili kuweza kutambua ni
aina gani ya dawa za kulevya, lakini bado tunaendelea na mahojiano naye
ili kubaini ni wapi amechukua unga huo,” alisema Otieno.
Kamanda
Otieno alisema kuwa kukamatwa kwa mtuhumuwa huyo kunatokana na
kuongezeka kwa udhibiti na kupata mashine za kisasa za utambuzi, ikiwa
ni pamoja na ari ya kazi. Tukio hilo limetokea wakati taifa na dunia,
inaadhimisha upigaji vita wa dawa za kulevya. Tukio hilo ni la kwanza
kwa mwaka huu katika uwanja huo.
|
0 maoni:
Chapisha Maoni