Mchezo wa pili wa Shirikisho la Afrika wa Yanga ambayo inataraji kuwa mwenyeji wa TP Mazembe katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam umetangazwa kuwa ni bure kwa mashabiki wa soka ili waweze kushangilia kwa wingi na kuisapoti timu hiyo.
Taarifa za kiingilio kuwa bure katika mchezo huo zilitolewa na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro na kueleza kuwa wamemua kuwapa mashabiki wa soka nchini nafasi ya kutizama mchezo huo ili kuishabiki Yanga ambao ndiyo wawakilishi pekee wa Tanzania katika mashindano ya kimataifa.
Muro alisema kuwa “Sisi ni watanzania tunataka kuionyesha dunia kuwa sisi ni wamoja, hata mashabiki wa Simba tunawakaribisha wavae jezi za Yanga au wakishindwa wavae jezi za taifa na hilo likiwa gumu wavae jezi za Simba na waje kuishabikia Yanga”
“Kama ulikuwa mkoani na unataka kuja kulipia VIP basi pesa yako tumia kama nauli ya kuja Dar es Salaam na kiingilio kitakuwa bure ili upate nafasi ya kuishangilia Yanga”