——————–
Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo limepitisha muswada wa
marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma wa Mwaka 2016 wenye lengo la
kupunguza gharama na muda wa mchakato wa manunuzi Serikalini.
Marekebisho
hayo yametokana na gharama kubwa ambayo Serikali imekuwa ikitumia
kutokana na huduma na Bidhaa zinazonunuliwa na Serikali kuwa za juu
ikilinganishwa na bei ya wastani ya soko.
“Muswada
wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma wa mwaka 2016 una lengo la
kuongeza ufanisi katika ununuzi wa Umma kwa kuondoa mapungufu yaliyopo
katika Sheria ya sasa kwa kupunguza gharama na muda wa michakato ya
ununuzi, kutoa upendeleo kwa kampuni za ndani, vikundi maalum, malighafi
na bidhaa zinazozalishwa nchini pamoja na kuweka viwango mahsusi kwa
bidhaa zitakazotumiwa na Serikali,” alifafanua Mwanasheria Mkuu wa
Serikali Mhe. George Masaju.
Mhe.
Masaju ameendelea kwa kusema kuwa sheria hiyo imeweka kifungu cha
dharura ili kuwezesha vitu vya kuokoa uhai na vinginevyo kununuliwa kwa
dharura pindi inapobidi.
Kwa
upande wake Mbunge wa Babati Vijijini Mhe. Jitu Soni yeye ameiomba
Serikali kuruhusu kununua vifaa tiba vilivyotumika ambavyo muda wake wa
kutumia hauna mwisho, kwa mfano vitanda vya kujifungulia ili kupunguza
gharama ya kununua vitanda vipya na kuweza kununua vitanda vingi kwa
wakati mmoja.
Aidha
Mhe. Jitu ameiomba Serikali kuirudisha tena Sheria hiyo Bungeni baada
ya mwaka mmoja ili kufanyiwa marekebisho na kuziba mianya yote ambayo
itakuwa imebainika mara baada ya utekelezaji wake kuanza.
Muswada
wa marekebisho ya sheria hiyo yanasubiri kusainiwa na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli ili kuanza utekelezaji
wake.
0 maoni:
Chapisha Maoni