Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene |
JUMLA ya wanafunzi 90,248 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha tano
na vyuo vya ufundi mwaka 2016 ambapo kati yao wasichana ni 28,911 na
wavulana 36,050. Hata hivyo, jumla ya wanafunzi 24,258 sawa na asilimia
27.2 wenye sifa wamekosa nafasi za kujiunga na kidato cha tano kutokana
na ufinyu wa nafasi za shule hizo.
Matokeo ya uchaguzi wa wanafunzi hao yalitangazwa jana na Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),
George Simbachawene (pichani) na kubainisha kuwa jumla ya shule 326
zikiwemo mpya 47 zimepangiwa wanafunzi wa kidato cha tano.
Aliagiza wanafunzi wote kuripoti katika shule walizopangiwa kabla ya
Julai 25, mwaka huu na kwamba mwanafunzi atakayechelewa kuripoti nafasi
yake itachukuliwa na aliyekosa nafasi. Alisema idadi hiyo imeongezeka
kwa wanafunzi 9,958 sawa na asilimia 18.1 ikilinganishwa na wanafunzi
55,003 waliochaguliwa mwaka 2015.
Kati ya wanafunzi waliochaguliwa 34,064 wakiwemo wasichana 13,466 na
wavulana 20,598 sawa na asilimia 52.4 watajiunga na masomo ya sayansi na
hisabati, wanafunzi 30,897 wakiwemo wasichana 15,445 na wavulana 15,542
sawa na asilimia 47.56 wamechaguliwa kusoma masomo ya sanaa na
biashara.
Jumla ya wanafunzi 393,734 wakiwemo wasichana 200,919 na wavulana
192,815 walihitimu kidato cha nne mwaka 2015. Kati yao, wanafunzi 90,380
wakiwemo wasichana 36,005 na wavulana 54,375 walifaulu daraja la kwanza
hadi la tatu sawa na asilimia 22.95 ya wanafunzi wote.
Akizungumzia wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na vyuo vya ufundi
alisema jumla ya wanafunzi 759 wakiwemo wasichana 220 na wavulana 539
wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya ufundi, idadi ya wanafunzi hao
imeongezeka kwa wanafunzi 280 sawa na asilimia 58.46 ikilinganishwa na
wanafunzi 479 waliochaguliwa mwaka 2015.
Aidha kutokana na ufaulu kuongezeka, idadi ya wanafunzi wa kike
waliochaguliwa kujiunga na vyuo hivyo imeongezeka kutoka wanafunzi 147
mwaka 2015 hadi wanafunzi 220 mwaka 2016 sawa na ongezeko la wanafunzi
73 ambao ni sawa na asilimia 49.66 Alisema wanafunzi hao ndio
walishindanishwa kwenye uchaguzi wa kujiunga na kidato cha tano na vyuo
vya ufundi kwa mwaka 2016 na walionekana kuwa na sifa za kuchaguliwa
kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi kwa mwaka 2016, sifa hizo
ni pamoja na kuwa na ufaulu wa krediti tatu na usiopungua daraja la
tatu pointi 25.
Akizungumzia taratibu za uchaguzi wa wanafunzi hao alisema kulingana
na utaratibu uliowekwa na serikali, mwanafunzi mwenye sifa za
kuchaguliwa kuendelea na kidato cha tano na vyuo vya ufundi ni yule
aliyejaza fomu ya uchaguzi.
Alisema kwa kutumia fomu hiyo mwanafunzi hujaza machaguo matano ya
tahasusi (combinations) kwa masomo anayotaka kusoma na shule
anayotarajia kujiunga nayo kwa kila chaguo.
Kuhusu wanafunzi waliokosa nafasi, Waziri Simbachawene alisema jumla
ya wanafunzi 24,528 sawa na asilimia 27.2 ya wenye sifa wakiwemo
wasichana 6,789 na wavulana 17,739 wamekosa nafasi ya kujiunga na kidato
cha tano na vyuo vya ufundi kutokana na ufinyu wa nafasi za shule za
kidato cha tano.
Alisema katika idadi hiyo kuna wanafunzi 348, wasichana 120 na
wavulana 228 wana umri zaidi ya miaka 25 ambao wanakosa sifa za
kuchaguliwa na wanafunzi 625, wasichana 323 na wavulana 302 wamekosa
tahasusi. “Wanafunzi hawa watadahiliwa na Baraza la Taifa la Ufundi
(NACTE) kwenye fani mbalimbali ambazo ni ualimu.
Afya, maendeleo ya jamii, kilimo, Aidha Tamisemi itafanya uchaguzi wa
pili (second selection) mara tu baada ya muda waliopewa wanafunzi
kuripoti shuleni kupita,” alisema.
Kuhusu wanafunzi kuripoti shuleni Waziri huyo alisema muhula wa
kwanza kwa wanafunzi wa kidato cha tano mwaka 2016, utaanza Julai 11,
mwaka huu kwa kuwa uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano
umefanyika kwa kutumia mfumo wa kompyuta kwa kuzingatia machaguo ya
wanafunzi ya tahasusi, ufaulu na nafasi zilizopo katika shule husika.
“Naagiza wanafunzi wote kuripoti kwa muda uliopangwa la sivyo nafasi
zao zitachukuliwa na walikosa nafasi hizo,” alisema na kuongeza kuwa si
kila anayepangiwa shule za serikali huripoti na ifikapo Julai 27, mwaka
huu watapitia na kuangalia nafasi ngapi zimeachwa wazi ili wale
walioachwa wapate nafasi.
Alitoa mwito kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa
Halmashauri, Miji, Manispaa na Majiji kuhakikisha kwamba azma ya
serikali ya kila tarafa kuwa na shule ya kidato cha tano inatekelezeka
ili kuwawezesha wanafunzi wote waliofaulu kupata nafasi ya kuendelea na
masomo ya kidato cha tano na sita.
“Kutokana na ongezeko la ufaulu wa masomo ya sayansi, ninahimiza
shule zitakazoanzishwa za kidato cha tano ziwe na vyumba vitatu vya
maabara za masomo ya sayansi ili kuongeza idadi ya wanafunzi wa tahasusi
za sayansi ambao ufaulu wao unakuwa bora zaidi kila mwaka,” alisema na
kuwahimiza pia wadau wa elimu kuhakikisha shule zote zinazoanzishwa kwa
ajili ya kidato cha tano zinakuwa za bweni kwa kuwa shule hizo ni za
kitaifa na zinatakiwa kupokea wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Awali Simbachawene alisema Tamisemi ina jukumu la kusimamia, kuratibu
na kufuatilia shughuli za elimu kwenye mamlaka za serikali za Mitaa
kuanzia ngazi ya elimu ya awali, msingi na sekondari.
Alisema kuanzia mwaka 2014 uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na
kidato cha tano na vyuo vya ufundi ni moja ya majukumu yanayosimamiwa na
Tamisemi baada ya kugatuliwa kutoka Wizara ya elimu sayansi na
teknolojia. Simbachawene alisema kazi za Wizara ya Elimu ni kutunga sera
ya elimu, mitaala, kusimamia ubora wa elimu kwa shule za serikali,
mashirika ya dini na watu binafsi.
0 maoni:
Chapisha Maoni