——————————
Serikali kupitia Mamlaka ya
Chakula na Dawa (TFDA) imesema hivi karibuni itaanza msako mkali wa
kuwatafuta na kuwakamata wauzaji wa dawa zinazokatazwa pamoja na
vipodozi vikali ambao wanajitangaza kupitia mitandao mbalimbali ya
kijamii.
Hayo yamesemwa na Meneja
Mawasiliano na Uhusiano wa Umma kutoka TFDA Bi. Gaudensia Simwanza
wakati wa mahojiano na mwandishi wa habari hii kuhusu kuibuka kwa watu
wanaotangaza biashara ya dawa na vipodozi ambavyo Serikali imevipiga
marufuku.
Akitaja bidhaa hizo Bi. Simwanza
alisema ni pamoja na dawa za kuongeza ukubwa wa viungo vya mwili,
kupunguza uzito wa mwili na vipodozi vyenye kemikali za kuchubua ngozi
bidhaa ambazo zinasababisha madhara makubwa kwa binadamu ikiwemo ugonjwa
wa Saratani.
“Kumezuka wafanyabiashara holela
wanaotumia mitandao ya kijamii kama vile Instagram, Facebook, Whatsup
Groups na kwengineko kutangaza biashara ya dawa na vipodozi vyenye
kemikali hatari ambavyo vimepigwa marufuku na TFDA hivyo wanaohusika
wajiandae, hivi karibuni tutaanza kuwashughulikia.” Alisema Simwanza.
Alibainisha kuwa bidhaa hizo
nyingi hazijathibitishwa na kupewa kibali na TFDA hivyo wauzaji
wanakiuka Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Sura ya 219 inayowataka
wafanyabiashara wote wa bidhaa hizo kuzisajili kabla hazijaenda kwa
mtumiaji na kutofanya hivyo ni kwenda kinyume na Sheria.
Alieleza kuwa TFDA kwa
kushirikiana na Jeshi la Polisi wameandaa mkakati madhubuti wa
kuhakikisha wanawabaini na kuwakamata wafanyabiashara wote wanaouza dawa
na vipodozi hivyo kupitia mitandao na kuwachukulia hatua ikiwemo
kuwafikisha mahakamani au kuwatoza faini.
“Wengi wa wafanyabiashara hao
hawaweki anuani za maeneo wanayopatikana na hawana maduka rasmi bali
huweka namba za simu za mkononi lakini kwa kutumia vyombo vya dola
tutawabaini tu na kuwatia mbaroni.” Alisisitiza Simwanza.
Kwa upande wake Meneja Mawasiliano
wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Bw. Innocent Mungy
amewatahadharisha watumiaji wa huduma za mawasiliano hasa matangazo ya
biashara kuwa makini na matangazo hayo kwani baadhi ya wafanyabiashara
hizo wanaweza kuwa ni watu wenye nia mbaya.
Hivi karibuni kumeibuka wimbi la
wafanyabiashara wa dawa mbalimbali pamoja na vipodozi ambao
wanajitangaza kupitia mitandao ya kijamii na kuna baadhi ya watu
wananunua bidhaa hizo bila ya kuhakikisha usalama wake jambo ambalo ni
hatari kwa afya zao.
0 maoni:
Chapisha Maoni