Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa, akihutubia wadau wa Jumuiya ya Benki za Wananchi
kutoka mikoa yote nchini (hawapo pichani), katika ukumbi wa Mikutano
wa Kambarage ulioko katika Jengo la Hazina Mjini Dodoma
Wadau
wa sekta ya Benki za Wananchi kutoka mkoani Mwanza, wakisikiliza kwa
makini mada zilizotolewa kuhusu uanzishwaji wa benki hizo nchini, katika
mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Kambarage ulioko katika Jengo la
Hazina mjini Dodoma
Wakiri
Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, akisalimiana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Benki za wananchi nchini, Bi. Elizabeth Makwabe, baada ya kufunguliwa
rasmi kwa mkutano huo uliowashirikisha viongozi wa mikoa mbalimbali
nchini katika ukumbi wa Kambarage, Jengo la Hazina mjini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, (Kushoto) akibadilishana
mawazo na Mkuu wa mkoa wa Singida, Mhandisi Mathew Mtigumwe, mara baada
ya kufunguliwa kwa mkutano wa siku moja wa wadau wa Jumuiya ya Benki za
wananchi, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kambarage, ulioko
katika jengo la Hazina Mjini Dodoma
(Picha zote na Benny Mwaipaja, WFP)
………………………………………………………………………………………………………….
Na Benny Mwaipaja-WFP
WAZIRI MKUU, Mhe. Kassim
Majaliwa, amezishauri taasisi za fedha nchini zipunguze viwango vya riba
zinazotoza kwenye mikopo ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi hususan
waishio vijijini kujikwamua kiuchumi
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo
Juni 15, 2016, wakati akifungua mkutano wa wadau wa Jumuiya ya Benki za
Wananchi (COBAT), ulioshirikisha viongozi wa mikoa 28 nchini,
uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Hazina Mjini Dodoma.
Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa amesema
kuwa riba kubwa inayotozwa na taasisi hizo za fedha ni kubwa na
kuwafanya wananchi wengi washindwe kunufaika na fursa za mikopo
inayotolewa, hali inayowafanya waendelee kuwa masikini.
“Kama Benki zitatoa mikopo yenye
riba nafuu, kila mwananchi atamudu kupata mtaji na kufanya biashara yake
akijua kuwa riba si kubwa na tayari Serikali imeanza kufanya mazungumzo
na taasisi za fedha kuhusu jambo hili ili ziweze kufanya mapitio ya
riba zake”Aliongeza Mhe. Kassim Majaliwa
Ameipa mikoa ambayo haijaanzisha
benki za wananchi-COBAT, muda wa miezi mitatu kuanzisha mchakato huo ili
kufikisha huduma rasmi za kifedha kupitia benki hizo ili kuchochea na
kuamsha uzalishaji mali wenye tija katika jamii.
Amesema lengo muhimu la kuwainua
wananchi kimaisha litatimia kwa kuhamasisha wananchi mijini na vijijini,
wenye kipato cha chini kabisa katika kujenga utamaduni wa kujiwekea
akiba na kuwekeza katika hisa ili kukuza mitaji itakayosaidia shughuli
za maendeleo kwenye maeneo yao yote.
Ameahidi kuwa Serikali itaangalia
uwezekano wa kuiwezesha mikoa itakayoonesha ari zaidi ya kuanzisha
benki zao za wananchi kwa kuzishirikisha Halmashauri za wilaya,
Manispaa, Miji na Majiji.
“Inawezekana kabisa kuanzisha
benki hizo kwa kukusanya hisa kutoka kwa wananchi na Halmashauri
zikachangia ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kufikiwa na huduma za
kibenki katika maeneo yao”Alisisitiza Waziri Mkuu.
Amesema ni matumani ya serikali
ya awamu ya tano kwamba uanzishwaji wa benki hizo una umuhimu mkubwa kwa
kuwa zitakuwa kiunganishi mahsusi ambacho kikiwa imara kitaleta
mabadiliko chanya katika kuwawezesha wananchi kujikwamua na kujiletea
maendeleo ya haraka.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Mpango, ameeleza kuwa hadi kufikia mwaka 2016, mikoa 8 tu ya
Tanzania bara ndiyo imeanzisha benki za wananchi-COBAT kati ya mikoa 26
iliyopo.
Amezitaja benki hizo zilizoko
chini ya Jumuiya ya Benki za Wananchi Tanzania-COBAT kuwa ni Mucoba
(Mufundi), Mbinga (Mbinga), Mwanga (Mwanga), Uchumi (Moshi), Tandahimba
(Mtwara), Meru (Arusha), Njombe (Njombe) na Efatha (Dar es salaam)
Dkt. Mpango amesema kuwa Benki
hizo zinawateja wanaokadiriwa kufikia 600,000 zikiwa na jumla ya mali
iliyofikia shilingi Bilioni 86.3 na amana za wateja shilingi Bilioni
69.2 na kutoa mikopo kwa wateja wake inayofikia shilingi Bilioni 56.2
“Mpango wa kuhakikisha huduma za
fedha zinawafikia wananchi wengi zaidi ni sehemu ya utekelezaji wa Dira
ya Maendeleo ya taifa inayolenga kuipeleka Tanzania katika nchi ya
kipato cha kati na yenye uchumi imara ifikapo mwaka 2015” Amesisitiza
Dkt. Mpango
Amesema hadi kufikia Desemba
mwaka 2015, Taasisi za benki za wananchi za mikoa, vyama vya ushirika
vya akiba na mikopo, zimeongezeka hadi kufikia 4,093, zikiwa na
wanachama 733,876 na kuwekeza kiasi cha shilingi Bilioni 377.6
“Aidha, Asasi za Fedha za Kijamii
(Vicoba, Vsla, Rosca), zinakadiriwa kufikia 100,000 na zina wanachama
milioni 2.2 na mtaji wa shilingi Trilioni 1.2” aliongeza Dkt Mpango
Amesema kuwa utafiti uliofanyika
hivi karibuni na shirika la Finscope umebaini kuwa asilimia 57.4 ya
watanzania wanapata huduma rasmi za kifedha, ambapo kati ya hao,
asilimia 13.9 wanapata huduma za kibenki huku asilimia 43.5 wanapata
huduma za kifedha zisizo za kibenki.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Mpango, amezitaja changamoto zinazoikabili sekta ya Fedha
nchini kuwa ni upungufu wa mitaji, ukusanyaji mdogo wa amana, kiwango
cha riba kuwa juu, ushindani kutoka benki za biashara na taasisi zingine
za Fedha, kukosekana kwa wataalamu wa kuziendesha na kukosekana kwa
sheria na kanuni mahsusi kwa benki za wananchi na Ushirika.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Benki za Wananchi Tanzania-COBAT, Elizabeth Makwabe, amesema
kuwa katika kipindi cha miaka 20 sasa, benki za wananchi zimeendelea
kupanua huduma zake ambapo hadi sasa, mali, amana na mikopo vimeongezeka
kutoka shilingi Bilioni 71.2 mwaka 2014 hadi kufikia shilingi Bilioni
86.3 mwaka 2015
Ameiomba serikali kuwekeza fedha
za kutosha kwenye benki za wananchi katika mfumo wa fedha za kuzungusha
(Revolving Fund) ili kusisimua uchumi katika maeneo ya vijijini pamoja
na kuzitaka Halmashauri za wilaya kuwekeza mitaji kwenye benki hizo
katika maeneo yao.
Akitoa neno la Shukrani kwaniaba
ya wakuu wa mikoa waliohudhuria mkutano huo, mkuu wa mkoa wa Manyara,
Dkt. Joel Bendera, ameahidi kuwa mikoa yote 18 ambayo haijaanzisha benki
za wananchi itahamasisha na kuanzisha benki hizo kwa faida ya wananchi
wao.
0 maoni:
Chapisha Maoni