Alhamisi, 16 Juni 2016

Matukio ya Ubakaji wa Watoto yafikia 2358 kwa Mwaka

images
Jonas Kamaleki-Maelezo- Dodoma
MATUKIO ya ubakaji watoto yameongezeka hadi kufikia 2358 kwa mwaka 2015 ikilinganishwa na 422 ya mwaka 2014 na kufanya vitendo hivyo kuwa tishio kwa watoto nchini.
Hayo yalibainishwa leo mjini Dodoma na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu kwenye mkutano na waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika.
“Asilimia 49 ya unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto hufanyika majumbani, wakati asilimia 23 hufanyika njiani wakati wa kwenda au kutoka shule na asilimia 15 hufanyika shuleni,”alisema Ummy.
Akionyesha kusikitishwa na ongezeko hilo la vitendo viovu dhidi yawatoto, Ummy alisema kuwa hali hii inatisha na kukera kwani ndani ya miezi mitatu mwaka huu yaani januari hadi Machi 2016 matukio 1765 yameripotiwa katika vituo mbalimbali vya polisi.
Aidha, Ummy alisema kuwa Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifali linaloshughulikia masuala ya watoto (UNICEF) ilifanya utafiti kuangalia hali halisi ya Ukatili dhidi yawatoto na kubaini kuwa wasichana 3 kati 10 na mvulana mmoja kati ya 7, wamefanyiwa ukatili wa kingono angalau mara kabla ya kutimiza miaka 18.
Kwa mujibu wa Wazirti Ummy alisema Utafiti huo pia umeonyesha  kuwa wasichana  4 kati ya 10 na wavulana 3 kati ya 10 wamefanyiwa ukatili zaidi ya mara tatu kabla ya kufikisha miaka 18, na wasichana 6 kati ya 10 wamefanyiwa ukatili ndani ya familia zao na msichana mmoja hadi wawili wamefanyiwa na walimu wao.
“Msikubali kuwalaza chumba kimoja watoto wa kike na ndugu wa kiume kwani tabia hizo chafu zimekuwa zikifanywa na watu wa familia,” alisema Ummy.
Aliongeza kuwa vitendo vya ubakaji na  ulawiti kwa watoto vina athari kubwa sana katika ustawi wa watoto..
Aidha alisema kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira  mazuri ya kisera na kisheria katika kusimamia utekelezaji wa haki ya motto ya kuishi, kulindwa na kuendelezwa, ikiwemo na kufanya mabadiliko ya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 inayohalalisha motto wa miaka 15 kuolewa kwa ridhaa ya wazazi na wa miaka 14 kwa kibali cha mahakama,” alisema Ummy.
Alisisitiza kuwa muswada wa Sheria ya Ndoa inabidi uletwe bungeni haraka iwezekanavyo na kuongeza kuwa mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria hiyo yameshapelekwa katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

0 maoni:

Chapisha Maoni