…………………………………………………………………………………………………..
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah Kairuki
(Mb) amewataka Watumishi wa Umma kuacha tabia ya kusambaza Nyaraka za
Siri za Serikali katika Mitandao ya Kijamii.
Waziri Kairuki aliyasema hayo katika kikao kazi cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mkoani Manyara.
Waziri Kairuki alisema serikali
inao utaratibu wake wa kusambaza nyaraka kwa waajiri, na taarifa
kumfikia kila mhusika na sio kupitia mitandao ya kijamii.
“Nawakumbusha kuhusu Kanuni za
maadili katika Utumishi wa Umma ambazo kila mtumishi anapaswa
kuzingatia na kuelewa na endapo kama huelewi uliza ueleweshwe” Waziri
Kairuki alisema na kuongeza Sheria, Taratibu na Kanuni za Utumishi wa
Umma lazima zifuatwe.
Aliongeza, hatua zitachukuliwa kwa wote watakaobainika kusambaza nyaraka kinyume na taratibu, kupitia namba zao za simu.
Waziri Kairuki, pamoja na mengine
alisisitiza waajiri kuwashirikisha Watumishi katika bajeti kupitia
baraza la wafanyakazi ili wajue mambo ya msingi watakayotekeleza na
kuweza kuhoji pale itakapolazimu kufanya hivyo na kwa Waajiri ambao
hawajaunda mabaraza ya wafanyakazi wameelekezwa kuunda mabaraza hayo.
Pia, Waziri Kairuki alikumbusha
kuwa uhamisho usifanyike kiholela, bali kwa sababu za msingi na pale
kibali cha ajira kinapotolewa utekelezaji ufanyike mapema ili huduma
ziendelee kutolewa.
Aidha, watumishi wanaoteuliwa katika nafasi za madaraka wathibitishwe katika kipindi cha miezi sita.
Pamoja na kupata fursa ya
kuongea, na kushauri, Watumishi wa Umma waliandika kero na maoni ambayo
yalichukuliwa ili kufanyiwa kazi.
Kikao hicho kilikua na lengo la
kupokea maoni na kero za watumishi wa umma ikiwa ni sehemu ya
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2016 na kilihudhuriwa na
watumishi wote wa mkoa wa Manyara, kupitia uwakilishi.
Wiki ya Utumishi wa Umma ni moja
ya tukio muhimu katika kalenda ya Umoja wa Afrika (AU), ambayo
huadhimishwa kutambua mchango wa watumishi wa Umma barani Afrika katika
kuleta maendeleo, ikiwamo kutatua changamoto zinazowakabili katika
kutekeleza majukumu. Wiki hii huadhimishwa na nchi wanachama wa Umoja wa
Afrika kwa wakati mmoja.






0 maoni:
Chapisha Maoni