Jeshi
la Polisi nchini, linatarajia kufanya uzinduzi wa mpango wa kuboresha
usalama wa jamii na mali zao, ambao una dhamira ya kupunguza uhalifu
nchini. Mpango huu utaanza kutekelezwa katika mkoa wa kipolisi wa
Kinondoni kuanzia mwezi wa Julai mwaka huu na baadaye kuufikisha katika
mikoa yote nchini mwanzoni mwa mwaka 2017.
Uzinduzi huo utafanyika siku ya
Jumamosi, tarehe 25 Juni, 2016 katika viwanja vya Biafra, Kinondoni Dar
es Salaam, kuanzia saa tatu asubuhi, ambapo Mgeni Rasmi katika uzinduzi
huo atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu
wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Mhe. Dr John Joseph Pombe Magufuli.
Sambamba na uzinduzi huo wa mpango, Mhe. Rais ataanza kuzindua kituo cha
Mawasiliano ya simu za dharura za Polisi 111, na 112 (Police Call
Centre) na kituo cha Polisi cha kuhamishika kilichopo maeneo ya Coco
beach mkabala na jengo la Coco Plaza, ambacho ni miongoni mwa vituo 13
vitakavyowekwa kwenye maeneo tete kiuhalifu yaliyoainishwa katika mkoa
wa kipolisi wa Kinondoni.
Lengo la Mpango huu ni kuimarisha
usalama wa wananchi katika jamii na mali zao. Huu ni ubunifu wa Jeshi
la Polisi katika kutekeleza majukumu yake ambapo Jeshi la Polisi
limeamua kuondokana na utendaji wa kimazoea kwa kuanzisha mikakati
mikuu minne ambayo ni kuongeza ufanisi katika shughuli za kipolisi,
kuongeza ubora katika utoaji wa huduma za kipolisi, kuimarisha
mawasiliano na ushiriki wa wadau pamoja na kubuni vyanzo mbalimbali
katika kutafuta rasilimali fedha.
Kupitia mikakati hiyo, Jeshi la
Polisi litaanzisha mpangilio mpya wa ulinzi na doria katika maeneo
yaliyokithiri kwa uhalifu, litaboresha Vituo vya Polisi kuwa katika
muonekano bora na wa aina moja nchi nzima, litaimarisha ubia na sekta
binafsi za ulinzi, litaongeza uharaka wa kufika kwenye matukio ya
uhalifu yanayoripotiwa, litaimarisha na kudumisha misingi ya maadili,
litaweka mifumo thabiti ya kusimamia rasilimali watu, litaimarisha
mawasiliano ya ndani na nje ya Jeshi, na mwisho litatafuta vyanzo
mbadala vya fedha zinazohitajika ili kuliwezesha Jeshi la Polisi
kutekeleza wajibu wake. Vyanzo mbadala vitaongeza wigo wa kutafuta
rasilimali fedha kutokana na ufinyu wa Bajeti ya Serikali ambayo Jeshi
la Polisi limekuwa likipata kila mwaka.
Aidha, uzinduzi huo utasindikizwa
na Wasanii mbalimbali wa Muziki wakiwemo, Bendi ya Polisi, ya Moto
Band, Manfongo, Ndolela, Man Prince pamoja na wasanii wengine na
burudani mbalimbali zitakuwepo.
Wananchi wote kwa ujumla
wanakaribishwa ili kupata maelezo ya kina na uelewa juu ya mkakati huu
mpya wa kimageuzi ulioandaliwa kwa kushirikiana na Ofisi ya
Rais-Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi (President’s Delivery
Bureau-PDB) inayoratibu Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Asanteni kwa kunisikiliza.
Imetolewa na:
Advera J. Bulimba – Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP)
Msemaji wa Jeshi la Polisi,
0 maoni:
Chapisha Maoni