Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa mwelekeo wa hali ya hewa kwa kipindi cha Juni hadi Agosti mwaka huu. Akizungumzia utabiri huo kwa mbo vya Habari mapema leo Jijini Dar es Salaam kuhusiana na mwelekeo huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Meneja Kituo Kikuu cha Utabiri Bw. Samwel Mbuya alisema  Tanzania inatarajia kuwa na hali ya baridi na vipindi vya mvua kwa maeneo machache ya nchi.
“Nchi yetu inatarajia kuwa na hali ya baridi kiasi katika kipindi hiki sambamba na vipindi vifupi vya mvua vinavyotarajiwa kujitokeza katika maeneo machache hususan ya ukanda wa Ziwa Viktoria na ukanda wa pwani ya Kaskazini (Visiwa vya Unguja na Pemba). Katika kipindi cha mwezi Juni hadi Agosti 2016, maeneo mengi ya nchi yanarajiwa kuwa makavu na yenye hali ya baridi kiasi katika majira haya ya kipupwe. ” alieleza Samweli Mbuya.
Meneja huyo ameongeza kuwa mifumo ya hali ya hewa inaonesha matarajio ya hali ya joto la wastani hadi chini ya wastani katika maeneo yaliyopo Kusini-Magharibi mwa nchi.
Hata hivyo, katika msimu wa Kipupwe wa mwaka huu maeneo mengi ya nchi yanatarajiwa kuwa na joto la wastani hadi juu ya wastani.
Meneja huyo amebainisha kuwa, hali ya ubaridi inatarajiwa zaidi nyakati za usiku hadi mapema asubuhi.  “Aliendelea kueleza sababu za hali hiyo kuwa ni pamoja  na  kupungua kwa joto la bahari katika eneo la ukanda wa Tropiki la bahari ya Pasifiki sambamba na Joto la baharí katika eneo la magharibi wa bahari ya Hindi  kuwa la wastani kwa kipindi cha miezi ya Juni hadi Agosti 2016.
Aidha, joto katika bahari ya Atlantiki linatarajiwa kuwa chini ya wastani. Hali hiyo inatarajiwa kusababisha upepo kuvuma kutoka magharibi ukielekea mashariki hususan katika maeneo ya Ukanda wa Ziwa Viktoria. Joto la bahari la juu ya wastani linatarajiwa katika eneo la ncha ya kusini ya bara la Afrika hivyo kuathiri msukumo wa upepo wa kusi.
Kwa upande wake, Afisa Uhusiano wa TMA, Bi. Monica Mutoni alitoa msisitizo kwa wananchi kufuatilia taarifa hususan za tahadhari zinazotolewa na Mamlaka kupitia vyombo mbalimbali vya habari, tovuti ya Mamlaka na vyanzo vingine vya habari ili kuokoa maisha na mali.
Bi. Monica aliongeza kuwa: “Hivi karibuni TMA imekuwa ikitoa tahadhari mbalimbali ikiwa ni pamoja na za kuwepo kwa upepo mkali na mawimbi makubwa kwenye ukanda wa Bahari Hindi, Maziwa na nchi kavu hivyo ni vyema wananchi hasa wale watumiaji wa bahari na maziwa kuchukua hatua stahiki pindi taarifa kama hizo zinapotolewa”.
Aidha, TMA ilipongeza sekta mbalimbali pamoja na Taasisi, Mamlaka za Serikali na jamii kwa ujumla  kwa hatua stahiki zilizochukuliwa katika kipindi cha msimu wa mvua za Masika 2016 kwa kutumia Taarifa, Agalizo na Tahadhari za utabiri zilizotolewa na Mamlaka. Ni wazi kuwa kwa hatua hizo madhara ambayo yangeweza kujitokeza yalidhibitiwa na hivyo kuchangia katika kufanikisha mipango na utekelezaji wa shuguli za kiuchumi na kijamii katika kipindi husika.
Hata hivyo, TMA inahimiza wananchi kutembelea kwenye tovuti ya TMA www.meteo.go.tz ama ofisi zao popote zilipo ili kupata taarifa kwa kina kuhusiana na mwelekeo wa hali ya hewa kwa kila mkoa.
Tazama MO tv, kuona tukio hilo hapa:

DSC_6944Meneja Kituo Kikuu cha Utabiri TMA, Bw. Samwel Mbuya akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa Habari (Hawapo pichani) wakati wa tukio hilo. Kulia ni Afisa Uhusiano wa TMA, Bi. Monica Mutoni
DSC_6941Mkutano huo kwa waandishi wa Habari ukiendelea
DSC_6943Meneja Kituo Kikuu cha Utabiri  TMA, Bw. Samwel Mbuya ( katikati) akitoa ufafanuzi wa taarifa hiyo  kulia ni Afisa Uhusiano wa TMA, Bi. Monica Mutoni na kushoto ni Afisa Habari wa Idara Habari MAELEZO, Bw. Frank Mvungi.
DSC_6935Afisa Uhusiano wa TMA, Bi. Monica Mutoni (kulia) akizungumza katika mkutano huo. Katikati ni Meneja Kituo Kikuu cha Utabiri  TMA, Bw. Samwel Mbuya na kushoto ni Afisa Habari wa Idara Habari MAELEZO, Bw. Frank Mvungi. (Picha zote na Andrew Chale,