Alhamisi, 16 Juni 2016

DAR, KIBAHA KUKOSA MAJI KWA SIKU TATU

SHIRIKA
LA Majisafi na Majitaka Dar es salaam (DAWASCO), imetangaza kuwapo tatizo la
upatikanaji wa huduma ya Maji katika maeneo yote yanayohudumiwa na mtambo wa
Maji wa Ruvu Juu, jijini Dar es salaam, pamoja na maeneo yote ya mji wa Kibaha
mkoani Pwani kutokana na mtambo huo kuzimwa kwa wastani wa saa 72, kuanzia siku
ya Ijumaa 17/06/2016, Jumamosi 18/06/2016 na Jumapili 19/06/2016.
Akizungumzia kukosekana Kwa huduma hiyo ya Maji,
Kaimu Meneja Uhusiano wa DAWASCO, Bi. Everlasting Lyaro, ameeleza  sababu ya kuzimwa kwa mtambo wa Ruvu Juu, ni
kumruhusu Mkandarasi (WABAG) kuunganisha mtambo mpya wa Maji na ule wa zamani,
ambapo baada kukamilika kwa kazi hiyo, uzalishaji wa Maji utaanza mara moja.
“Tuko kwenye hatua ya mwisho ya kuunganisha mtambo
mpya wa Maji na ule wa zamani, kazi hii ikikamilika, uzalishaji utapanda kutoka
wastani wa lita Milioni 70 hadi kufikia lita Milioni 106 kwa siku hivyo kuweza
kutimiza lengo letu la kumtua mama ndoo ya Maji kichwani” alisema Lyaro
Lyaro, ameeleza kuwa kuzimwa kwa mtambo huo,
kutasababisha maeneo ya
Mlandizi,
Kibaha, Kibamba, Mbezi, Kimara, Ubungo, Kibangu, Makuburi pamoja na eneo lote
la Tabata, Segerea hadi Kinyerezi kukosa huduma ya Maji.
Hivyo,
ametoa wito kwa wateja na wananchi wote kuhifadhi Maji ya kutosha na kuyatumia
kwa matumizi muhimu na lazima ili kukidhi mahitaji yao kwa kipindi  chote cha kukosekana kwa huduma hiyo.
 

 

0 maoni:

Chapisha Maoni