Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbawara, ameagiza kituo cha kuhifadhi kumbukumbu (Data centre) mbalimbali cha Kijitonyama jijini Dar-es-salaam kianze kufanya kazi mara moja, kwa madai kituo hicho muhimu kikiendelea bila kufanya kazi, kinaitia hasara kubwa serikali.
Waziri huyo ametoa agizo hilo wakati akikagua njia ya mkongo wa taifa eno la kijiji cha Iguguno wilaya ya Mkalama, Singida.
Alisema kituo hicho kwa sasa kinaendelea kuitia hasara serikali kwa kuingia gharama mbalimbali ikiwemo ya umeme na mishahara ya wafanyakazi kutokana na kutokuanza kazi, wakati kimekamilika kujengwa muda mrefu.
“Sielewi kuna sababu gani inakwamisha kituo hicho kuanza kazi wakati wateja wake wako wengi, na wanasubiri tu kituo kianze kufanya kazi. Pengine ni watumishi wake wanafanya kazi kwa mazoea … TTCL wanasuasua na katibu wangu mkuu, naye hasimamii kikamilifu kituo hichi ambacho ni kitega uchumi kikubwa cha serikali,” alisema.
Waziri Mbawara, alitumia fursa hiyo kumwagiza katibu wake mkuu upande wa mawasiliano,ahakikishe anasimamia kikamilifu mradi huo ili uanze mapema iwezekanavyo.
IMG_6217
Waziri wa ujenzi,uchukuzi na mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto) akipewa maelezo juu ya mitambo ya simu ya TTCL mjini Singida
“Mradi huu  serikali imeukopea fedha nyingi na zinatakiwa kurejeshwa kwa wakati. Sasa badala ya kituo kuanza kazi mapema, kimeendelea kubaki  bila kufanya kazi huku mambo yote muhimu,yameisha kamilika. Hatuwezi kuruhusu hali hii ya kuitia hasara serikali, iendelee,” alifafanua zaidi.
Kituo hicho ambacho karibu kila nchi duniani inacho, kinatarajiwa kuweka au kuhifadhi taarifa/kumbukumbu mbalimbali muhimu za taasisi za fedha, makampuni na wadau ili endapo taasisi itapoteza taarifa zake muhimu ikiwemo majengo kuugua moto,waweze kuzipata kwenye kituo hicho.
Katika hatua nyingine, Meneja wa TTCL kanda ya kati, Peter Lusama, alisema kampuni ya simu Tanzania (TTCL) mkoa wa Singida, imekusanya mapato yake zaidi ya shilingi 132 milioni sawa na asilimia 180 ya lengo kati ya Januari hadi Mei mwaka huu.
 Alisema mafanikio hayo yametokana na malipo mbalimbali kutoka kwa wateja 4,452 (1,490 wa simu za mezani, 2,932 wa simu za mkononi na wateja 30 walioungwa kupitia mkongo wa Taifa).
“Tukiangalia mwenendo wa mahitaji ya huduma  katika mkongo wa Satellite (Broad band) hasa mradi wa simu za mkononi unaotarajiwa  kuwa tayari mwezi huu wa Juni, tuna uhakika wa kuyapandisha mapato na kuweza kufikia lengo la mwaka huu, la zaidi ya shilingi 232.5 milioni,” alisema.
Hata hivyo, meneja Lusama  alisema pamoja na mafanikio hayo, wamekabiliwa na changamoto ya deni kubwa la zaidi ya shilingi 94.8 Milioni na taasisi za Serikali wameweka mikakati ya kuhakikisha deni hilo linalipwa mapema iwezekanavyo.
Aidha, meneja huyo alisema kama ilivyo kwa mikoa mingine, mkoa wa Singida nao unapata mawasiliano kupitia katika mkongo wa Taifa wenye urefu wa takribani Kilometa 433.
“Kati ya Kilometa hizo 433, Kilometa 153 zimechimbiwa chini ya ardhi na Kilometa 280 zinapita juu ya nguzo za TANESCO. Tunaendelea kutoa elimu kwa wadau wote vijijini vinavyopitiwa na mkongo wa Taifa, ili waendelea kuhakikisha usalama wa mkongo, unadumishwa,” alisema meneja huyo.
Lusama  alisema hata hivyo, hakuna matukio ya kuhujumu mkongo huo hadi sasa zaidi ya maeneo korofi katika njia ya chini ambayo tumeshayatafutia ufumbuzi wa kudumu.
Kwa mujibu wa Meneja huyo, TTCL Mkoa wa Singida, inahudumia Wilaya tatu kati ya tano zilizopo. Wilaya hizo ni Singida, Manyoni na Iramba, utoaji wa huduma katika wilaya mpya za Ikungi na Mkalama, ziko katika hatua za awali za ujenzi wa minara.
Na Nathaniel Limu