Kikundi
cha wajasirimali wanawake kutoka Tanzania (Tanzania Saccos for Women
Enterprenuers) kinachoongozwa na Bi. Anna Matinde Mkurugenzi wa Bodi ya
Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania waliwasili nchini Comoro kwa ajili ya
ziara ya siku mbili. Lengo la ziara hiyo ni kutafuta masoko kwa ajili ya
bidhaa za kutoka Tanzania, pamoja na kukutana na wajasiriamali wa
Comoro ili kuweza kubadilishana taarifa juu ya fursa mbalimbali za
biashara kati ya Tanzania na Comoro.
Wajasirimali
hao waliwasili nchini Comoro tarehe Juni, 13 na kupokelewa na Balozi
wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Chabaka F. Kilumanga. Wakati wakiwa
nchini Comoro, wajumbe walipata fursa ya kukutana na wajumbe kutoka
sekta binafsi ya Komoro pamoja na wa Tanzania waishio Comoro (Diaspora).
Ujumbe huo ulifurahishwa sana na fursa za biashara zilizopo Comoro
ambapo walielezea kuwa wapo tayari kushirikiana na Wakomoro katika
kuleta bidhaa mbalimbali katika soko la Comoro.
Aidha,
wajumbe walipata fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na Jumuiya ya
Watanzania waishio Komoro (TADICO). Katika majadiliano yao, wajumbe
waliweza kushaurina juu ya mikakati ya kufanya biashara nchini Comoro,
ambapo Bi. Matinde aliwaaelezea wanadiaspora wasisahu pia kuekeza
nyumbani kwani nako kuna fursa nyingi hivyo ni muhimu kwa wanadiaspora
kuangalia namna gani na wao wanaweza kunufaika na fursa hizo.
Wajumbe
pia walipata fursa ya kuonyesha na kutangaza biashara zao kwa
wafanyabiashara wa Comoro ambapo walionyeshwa kuvutiwa sana na bidhaa za
kutoka Tanzania. Ikumbukwe kwamba Comoro ni nchi ambayo hutegemea kwa
kiasi kikubwa bidhaa zake kutoka nje.
Biashara
kati ya Tanzania na Comoro imekuwa ikikuwa siku hadi siku hata hivyo,
bado kuna mahitaji makubwa ya bidhaa za chakula na imeonekana kuwa
Tanzania ndio nchi iliyo katika nafasi nzuri kukidhi mahitaji hayo,
kutokana na ukaribu wa nchi hizo kijiografia na kimila.
Wajasiriamali wa Comoro wakiangalia bidhaa kutoka Tanzania
Sambamba
na hilo, kikundi cha wajasirimali wanawake kutoka Tanzania wanatarajia
kutiliana saini mkataba wa ushirikiano (Memorandum of Understanding)
baina yao na vikundi mbalimbali vya wajasiriamali wa Comoro.
Katika
maelezo yake, Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Mhe. Chabaka Kilumanga
alieleza kuwa huu ndio wakati muafaka wa vikundi hivyo vikaanza kufanya
kazi kwa pamoja na kujuana ili kuweza kuboresha na kukuza wigo wa
biashara kati ya Tanzania na Comoro. Alieleza pia kuwa ubalozi
utaaendelea kushirikiana na wanadiaspora iwapo watapendelea kufanya kazi
kwa pamoja na wajasirimali hao.
0 maoni:
Chapisha Maoni