Kamati
ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), iliyopewa jukumu la
kusimamia uchaguzi wa Klabu ya Young Africans imeridhishwa na mwenendo
wa wanachama kwa namna wanavyochukua na kurejesha fomu.
Katika
kikao chake cha kufanya tathmini kilichoketi jioni ya leo Kamati hiyo
chini ya Mwenyekiti wake, Wakili Msomi Alloyce Komba kutokana na mipango
yake, imesogeza mbele mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu mpaka
Jumatatu Juni 6, 2016 saa 10:00 jioni. Isipokuwa Jumamosi na Jumapili ya
Juni 4 na 5, 2016.
Hadi
sasa wanachama tisa (9) wamechukua na kurejesha fomu. Wanachama hao ni
Aaron Nyanda na Titus Osoro wanaowania nafasi ya makamu mwenyekiti kwa
mujibu wa katiba ya mwaka 2010 inayotambulika serikalini hadi sasa.
Wengine
ni Paschal Laizer, Edgar Chibula, Mohammed Mattaka, Mchafu Ahmed
Chakoma, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ Omari Said kutoka Zanzibar ambao
wanawania nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji. Uchaguzi wa Yanga
unatarajiwa kufanyika Juni 25, 2016.
Fomu
zinapatikana katika ofisi za TFF zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu ya
Karume, Ilala jijini Dar es Salaam. Vilevile utaratibu unafanyika ili
fomu ziweze kupatikana katika tovuti ya shirikisho www.tff.or.tz
Fomu
zinapatikana kwa gharama ya Sh 200,000 kwa nafasi ya mwenyekiti na
makamu mwenyekiti na Sh 100,000 kwa wagombea wa nafasi ya ujumbe wa
kamati ya utendaji. Mwisho wa kuchukua na kurejesha fomu ni tarehe 6
Juni, 2016.
0 maoni:
Chapisha Maoni