Pichana na Benny Mwaipaja
Kaimu Msemaji wa Serikali Wizara ya Fedha na Mipango
…………………………………………………………………………………………………………………
Benny Mwaipaja, WFM-DODOMA
SERIKALI za Tanzania na Sweden
zimetiliana saini mkataba wa ushirikiano wa miaka 4 kuanzia mwaka 2016
hadi mwaka 2019 utakaojikita kuimarisha uchumi wa nchi na maendeleo ya
watu katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, utafiti, nishati jadidifu
na kupambana na umasikini.
Tukio hilo limefanyika leo Juni
16, 2016, mjini Dodoma kati ya Katibu Mkuu na mlipaji Mkuu wa Serikali,
Dkt. Servacius Likwelile kwa upande wa Tanzania na Naibu Waziri wa
Ushirikiano wa Kimaendeleo wa Sweden, Mhe. Ulrika Modeer.
Dkt. Likwelile ameeleza kuwa
katika kipindi cha kuanzia mwaka 2013 hadi mwaka 2019, Serikali ya
Sweden itatoa ruzuku ya fedha za Kiswidi, SEK 5.5 Biln, sawa na shilingi
Trilioni 1.42 za Kitanzania.
Amesema kuwa kutiwa saini kwa
mkataba wa ushirikiano huo kutafuatiwa na utiwaji saini wa mikataba ya
kifedha ambapo fedha hizo zitaelekezwa katika miradi kadhaa ikiwemo
kusaidia Elimu, Maendeleo ya Jamii-TASAF, Utafiti, Nishati, Demokrasia,
Haki za Binadamu, na Sekta Binafsi.
“Ushirikiano huu umelenga
kusaidia kujenga mazingira ya maendeleo endelevu na kuwapatia Watanzania
maskini fursa za kujikwamua katika umaskini kwa kujipatia ajira na
kuweza kuanzisha biashara za kujipatia kipato ambapo vikundi
vinavyolengwa zaidi ni wanawake, watoto na vijana” Alisema Dkt.
Likwelile
Dkt. Servacius Likwelile ametoa
wito kwa Serikali ya Sweden na nchi nyingine duniani kuwekeza katika
biashara na vitega uchumi ili ziweze kunufaika na rasimali kubwa ambazo
nchi imejaaliwa ikiwemo maliasili, ardhi yenye rutuba na jiografia ya
kimkakati inayochochea uwekezaji na biashara
Kwa upande wake Naibu Waziri wa
Ushirikianno na Maendeleo ya Kimataifa wa Sweden Mhe. Ulrika Modeer,
amepongeza uongozi mahili wa Rais wa Awamu ya Tano, Dkt. John Pombe
Magufuli kwa kupambana na vitendo vya kifisadi ikiwemo rushwa.
“Sweden inaunga mkono kwa nguvu
zote hatua zinazochukuliwa na Rais Magufuli kupambana na mauvu nchini na
tunaamini nchi itapiga hatua kubwa kimaendeleo” Alisistiza Modeer.
Mhe. Ulrika Modeer ameahidi kuwa
serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa kutoa fedha
kupitia mfuko mkuu wa Bajeti ili kuwezesha kufanikisha miradi mbalimbali
ya maendeleo inayogusa hifadhi ya mazingira, kilimo endelevu,
kuwawezesha wananawake kiuchumi na kumsaidia mtoto wa kike na kiume
kielimu.
“Tunataka kuona kuwa maendeleo ya
nchi yanakwenda sambamba na maendeleo ya wananchi wake ambapo tunaamini
kuwa utafiti utasaidia kupata njia bora za kupambana na
umasikini”Alisisitiza Mhe. Modeer
Amesema kuwa pamoja na nchi yake
kutaka kuyasaidia makundi mbalimbali wakiwemo watu wenye ulemavu,
wanataka kuona suala la demokrasia na utawala bora vinapewa kipaumbele
katika mipango mbalimbali ya maendeleo
“Vilevile uwekezaji wetu mkubwa
wa fedha katika maendeleo ya Taifa hautakuwa na maana sana kama suala la
hifadhi ya mazingira halitapewa kipaumbele kwa kuanzisha miradi ya
nishati jadidifu “Renewable energy” ili kukabiliana na mabadiliko ya
tabia nchi: aliongeza Mhe. Ulrika Modeer
Uhusiano wa Tanzania na Sweden
umedumu tangu mwaka 1960 ambapo katika kipindi chote cha miaka 50,
serikali hizi mbili zimeshirikiana katika kubuni na kutekeleza miradi
kadhaa ya maendeleo
Programu na miradi
itakayotekelezwa katika ushirikiano uliosainiwa leo unaendena pia na
Mpango wa Taifa wa Pili wa Miaka Mitano unaoanzia mwaka 2016/17 hadi
2020/21 na unalenga kuondoa utegemezi wa misaada kwa Tanzania.






0 maoni:
Chapisha Maoni