Alhamisi, 2 Juni 2016

MGODI WA BUZWAGI WAKABIDHI HUNDI YA MILIONI 588 KWA HALMASHAURI YA MJI WA KAHAMA

 
Mkuu wa Wilaya Kahama, Vita Kawawa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Kahama wakikabidhi mfano wa Hundi ya Sh Milioni 5888,842,728  kwa mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kahama Anderson Msumba,fedha zilizotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi kama ushuru wa Hudma (Service Levy)  kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya kisasa .wengine pichani ni Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi Mhandisi Asa Mwaipopo (kushoto) akishuhudia tukio hilo.
 
Mkuu wa wilaya ya Kahama Mh. Vita Kawawa akiwahutubia baadhi ya wananchi
(hawapo picha) na viongozi wakati wa hafla hiyo ya kupokea hundi
kutoka kwa Mgodi wa Buzwagi.
Mkurugenzi wa halmashauri ya
mji wa Kahama Anderson Msumba
akitoa neo la shukrani mara baada ya kukabidhiwa hundi.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama,Vita Kawawa akiteta jambo na Meneja
Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi unaomilikiwa na Kampuni ya Acacia, Mhandisi
Asa Mwaipopo
wakati wa hafla ya kukabidhi Hundi hiyo.
 
 
Kahama: Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi umeikabidhi halmashauri ya mji wa Kahama
hundi yenye thamani ya kiasi cha shilingi milioni miatano themanini na nane ikiwa
ni sehemu ya kodi ya huduma (service levy) katika kipindi cha kuanzia
Julai – desemba 2015.
Akikabidhi hundi hiyo kwa mkuu wa wilaya ya Kahama, katika hafla fupi iliyofanyika
katika uwanja wa taifa Kahama, Meneja mkuu wa Mgodi wa Buzwagi
Mhandisi Asa Mwaipopo amesema Kampuni yake imekuwa ikizingatia sheria
kwa kulipa kodi mbalimbali ambazo zimewekwa kwa mujibu wa sheria.
“Toka kuanza kwa shughuli zetu za uchimbaji mwaka 2009 mpaka 2015 mgodi wa
Buzwagi pekee umelipa kodi mbalimbali ambazo zinafikia kiasi cha
shilingi za kitanzania bilioni 197 kiasi hiki kinahusisha kodi na tozo
mbalimbali kama vile kodi ya huduma (service levy), Pay as you earn
(PAYE), kodi ya zuio (withholding tax), na kodi ya mrabaha”.alisema Mwaipopo.
  “Katika kodi hizi, kodi ya huduma (service levy) imekuwa ikilipwa
moja kwa moja kwa halmashauri ya mji wa Kahama ambapo mpaka mwisho wa
mwaka jana zaidi ya shilingi bilioni 3.4 sawa na asilimia mbili ya kodi
zote zimelipwa kwa halmashauri ya Kahama pekee.”aliongeza Mwaipopo.
Mwaipopo amesema licha ya Kampuni yake kulipa kodi mbalimbali bado
imekuwa ikijishughulisha katika kuhakikisha inakuwa mdau muhimu wa
maendeleomkwa kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo
yanayozunguka Mgodi.
“Mheshimiwa mkuu wa wilaya katika kipindi cha mwaka 2015 pekee takribani shilingi
bilioni moja nukta saba 1.7 zimetumika katika kutekeleza miradi
ya elimu, afya na maji na miradi yote hii ilelenga katika kuinua uchumi
wa wilaya pamoja na kuboresha ustawi wa maisha ya wenyeji.”alisema Mwaipopo.
“Acacia kupitia Mgodi wetu wa Buzwagi tunajivunia kuwa mdau muhimu wa maendeleo
kwa halmashauli ya mji wa Kahama na serikali kwa ujumla, na
tunafarijika sana kwa ushirikiano ambao tumekuwa tukiupata.”
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kahama Mh. Vita Kawawa aliyepokea hundi
hiyo kutoka kwa uongozi wa Buzwagi na baadae kuikabidhi kwa mwenyekiti
wa halmashauri ya Kahama ameupongeza uongozi wa Mgodi wa Buzwagi kwa
jitihada ambazo wamekuwa wakizifanya katika kuhakikisha wanashirikiana
na jamii katika kutekeleza miradi mbalimbali, huku akiwataka viongozi wa
halmashauri ya mji wa Kahama kuhakikisha pesa
hizo zinatumika kutekeleza miradi itakayokuwa na manufaa ya moja kwa
moja kwa Jamii.
“Ombi langu kwa wataalamu wa halmashauri na madiwani ambao ndio wasimamizi wa
pesa hizi kuhakikisha kuwa zinatumika kama zilivyokusudiwa na kwa
sababu safari hii tumeamua zijenge hospitali basi hakikisheni tunapata majengo
ya kisasa pamoja na vifaa tiba kwa manufaa ya watu wa Kahama”alisema Kawawa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Kahama Abel Shija
amesema wao kama madiwani watahakikisha kwamba pesa hizo zinatumika
katika utekelezaji
wa miradi iliyokusudiwa.
“Ndugu zetu hawa wa Mgodi wamekuwa wakilipa kodi hizi lakini wananchi wamekuwa
hawaoni kinachofanyika hali ambayo imepelekea minung’uniko miongoni
mwa wananchi, Kwa kuamua kuzitumia fedha katika ujenzi wa Hospitali ya
wilaya kila mtu ataona kinachofanyika na itasaidia kuondoa
minunung’uniko ambayo imekuwa ikijitokeza kutoka kwa wananchi”
Hafla hiyo pia ilisindikizwa na burudani ya mpambano mkali wa mpira wa miguu
baina ya timu za Mgodi wa Buzwagi na timu ya hospitali ya
wilaya mchezo ambao uliisha kwa timu ya hospitali ya wilaya kuibuka
mshindi kwa kuifunga timu ya Buzwagi 2-1.

0 maoni:

Chapisha Maoni