SERIKALI katika Wilaya ya
Wete , imemuomba Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar kuleta kikosi kazi
cha Polisi Kisiwani Pemba kwa ajili ya kusaidia upelelezi na
ukamatwaji wa watu wanaofanya hujuma za kuharibu vipando na mali za
wananchi .
Mkuu wa Wilaya ya Wete ,
Rashid Hadid Rashid aliyasema hayo baada kutembelea shamba la aliyekuwa
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Dadi Faki Dadi lililoko Finya Mianzini ,
kukatwa minazi 46 , mikarafuu 5 na mashina ya mihogo 51.
Mkuu huyo wa Wilaya ametoa ombi
hilo kufuatia vitendo hivyo kuongezeka kila uchao na kusababisha
hasara kwa wenye mali na Taifa kwa ujumla, jambo ambalo linaweza
kudhoofisha uchumi wa nchi na wananchi wake .
“Kutokana na kuongezeka kwa
matukio ya hujuma , iko haja kwa Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar
kuleta kikosi kazi kwa ajili ya kufanya upelelezi ili wahusika waweze
kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ”alisema Mkuu wa Wilaya
.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati na ulinzi na usalama amelaani vikali
vitendo hivyo vya hujuma vinavyofanywa na watu wasiojulikana na
kuvitaja kwamba ni njama za makusudi zinazofanywa na baadhi ya watu kwa
misingi ya itikadi za kisiasa .
Akitoa taarifa kwa kamati ya
Ulinzi ya Ulinzi na Usalama , Mlinzi wa Shamba hilo Ali Naulima Ulamu
alisema , hujuma hizo alizibaini baada ya kufika katika eneo hilo kwa
ajili ya shughuli za kilimo majira ya saa kumi na mbili (12) asubuhi .
Ulima alifahamisha kwamba bado
hajawabaini watu waliohusika na kitendo hicho ambapo , alichukua hatua
ya kumupa taarifa Sheha pamoja na mmiliki wa Shamba kuhusiana na hujuma
hizo .
“Nilibaini kuwepo na uharibifu
huu majira ya saa 12 asubuhi baada ya kufika kwa ajili ya shughuli za
kilimo , lakini nilichokifanya ni kutoa taarifa Serikalini pamoja na
kumpa taarifa mmiliki wa shamba ”alieleza.
Kwa upande wake mmiliki wa
shamba hilo Dadi Faki Dadi aliwataka wananchi kuwa na hofu ya Mungu kwa
kuhakikisha wanajiepusha matendo ambayo yanakinzana na Haki na Binadamu
na utawala wa misingi ya Sheria .
Alieleza kwamba ni jambo la
kushangaza kwa muumini wa dini kutekeleza vitendo vya kuhujumu mali za
mwenzake hasa katika kipindi hichi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa
Ramadhan .
Aidha amewashauri viongozi wa
dini kutumia fursa waliyonayo kwa kutenga muda wa kuyaungumzia matendo
hayo wakiwa katika sehemu zao Ibada , ili waumini waweze kutambua athari
zake .
Hili ni tukio la nane kutokea
katika Wilaya ya Wete la kuhujumiwa kwa mali , mazao na vipando vya
wananchi ikiwemo uchomaji moto nyumba , mashamba ya mikarafuu , majengo
ya Serikali , kufyekwa kwa mashamba ya mipunga na kung’olewa kwa vipando
baada ya kumalizika uchaguzi Mkuu wa marejeo uliofanyika machi 20
mwaka huu .
Tangu kuanza kutokea kwa
matukio hayo katika Wilaya hiyo , hakuna mtu au kikundi cha watu
waliokamatwa wakihusishwa na hujuma hizo .
0 maoni:
Chapisha Maoni