Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu wa Ufukweni (Beach soccer) inatarajia kuondoka siku ya Alhamisi kuelekea nchini Ivory Coast kwa ajili ya mechi ya marudiano na Timu ya Taifa ya nchi hiyo itakayofanyika siku ya Jumamosi.
Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Ufukweni, John Mwansasu amesema licha ya kufanya mabadiliko katika kikosi cha timu hiyo, pia ameongeza muda wa kufanya maandalizi ili kuwaweka sawa wachezaji kwa lengo la kupata matokeo mazuri ili timu iweze kufuzu.
“Maandalizi yako vizuri tunatarajia kuondoka siku ya Alhamisi, na kama hatutaondoka asubuhi nitaongeza muda wa kufanya mazoezi ili kuwaweka sawa wachezaji,” amesema.
Mwansasu amesema mechi ya awali timu ilikosa matokeo mazuri kwa sababu wachezaji hawakujiandaa vizuri kimwili na kiakili na kupelekea wachezaji hao kukosa pumzi kipindi cha pili na kuruhusu wapinzani kuutumia muda huo kupata magoli ya haraka.
“Hatukufanya maandalizi mema vya kutosha tulifanya siku mbili tu na ndiyo maana wachezaji hawakuwa na pumzi. Kwa kuutambua udhaifu huo tumeanza mazoezi toka Jumamosi iliyopita hivyo tuna muda mzuri wa kufanya mazoezi,” amesema.
Ameongeza kuwa “Tunategemea kupindua matokeo tumeongea na vijana kurekebisha kasoro zilizojitokea na kama tuliweza kufunga mabao 3 mfululizo kipindi ambacho hatukufanya mazoezi vizuri, tunaweza kufanya vizuri katika mechi ijayo kwa kuwa tumefanya mazoezi ya kutosha.”
Pia ametaja sababu za kumuongeza kipa Juma Kaseja katika kikosi chake kuwa anauwezo wa kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza katika mechi iliyopita.
“Nmewaongeza Banka na Kaseja kwa sababu ya makosa madogomadogo niliyoyaona, sababu Kaseja ni mzoefu na siyo mara ya kwanza kumuita hata kwenye mechi ya Kenya nilimuita kuja kuwafundisha wachezaji, halafu goli kipa ndiyo nguzo ya mafanikio na muanzishaji wa mashambulizi ya mchezo wote,” amesema na kuongeza.
“Unapokuwa na golikipa mzoefu ni rahisi kupata matokeo na kupata magoli mengi, kama tunataka kufuzu lazima tuwe na uwezo wa kufika golini haraka, hasa kwa mechi iliyokaribu yetu ambayo tunahitaji matokeo ili tufuzu,”
 Na Regina Mkonde