Mwakilishi mteule wa Chama cha
Alliance for Development Change (ADC) Hamad Rashid Mohammed, amemuomba
Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, atakapounda serikali achague
watendaji wenye utaalamu wanaoweza kuisaidia serikali kuinua uchumi
wake.
Akichangia hotuba ya Rais baada
ya kuapishwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, Rashid amesema kupewa
nafasi kwa wataalamu kutaisaidia serikali kufikia malengo inayojipangia
kwa kuwaletea maendeleo wananchi.
Mwakilishi huyo aliyegombea urais
wa Zanzibar kupitia ADC katika uchaguzi mkuu uliopita, amesema katika
kipindi cha pili cha awamu ya saba, Dk. Shein anahitaji wataalamu
wachumi na watakaotumikia nchi kwa uadilifu.
Aidha, alisisitiza vyombo vya
sheria vitumie nafasi yao dhidi ya watendaji na viongozi watakaokiuka
sheria na kujaribu kuikwamisha serikali kutimiza malengo yake.
Aliiomba serikali iache muhali
kwa kulea watendaji wasiotimiza majukunmu yao ipasavyo, akisema ni
lazima watu kama hao wachukuliwe hatua madhubuti vyenginvyo nchi itarudi
nyuma kimaendeleo.
Rashid alieleza kuwa,
kinachokwamisha nchi kupata maendeleo ni watendaji na viongozi wengi
kutojali wakati na kupoteza muda mwingi kwa mambo yasiyokuwa ya msingi
badala ya kufanya kazi.
“Tumeshuhudia watu wengi
wakkinyimwa au kucheleweshewa huduma wakiwemo wawekezaji wanaoomba
miongozo. Hili ni tatizo na lazima tufike wakati likomeshwe,”
alisisitiza.
Aliitaka serikali kuiga mfano wa
Tanzania Bara, ambapo amesema mtu anayeomba huduma hupangiwa mtendaji
maalumu wa kumsaidia, na pia hujulishwa mapema tarehe atakayomaliziwa
mchakato wake na kupewa majibu au kutumiwa kokote aliko.
Kwa upande mwengine, aliitaka
serikali iwe makini katika kusimamia ukusanyaji wa mapato kwani kodi
ndio msukumo wa kuharakisha maendeleo.
Rashid aliwataka wananchi
waondokane na fikra za kutegemea misaada kutoka nchi za nje, na badala
yake wakaze buti katika kufanya kazi za uzalishaji na huduma kwa kutumia
rasilimali zilizomo nchini.
Kwa upande wake, Mohammed Aboud
Mohammed ambaye pia ni mwakilishi wa kuteuliwa na Rais, amewaomba
wajumbe wenzake waache siasa kwani uchaguzi umekwisha na kilichobaki
sasa ni kujenga nchi.
Amefahamisha kuwa katika suala la
maendeleo, si vyema kuingiza itikadi za kisiasa, dini, ukabila au
maeneo watu wanakotoka kwani Zanzibar ni nchi ya Wazanzibari wote.
Aidha aliwataka wananchi wawe
watulivu, wavumilie na kushirikiana katika shughuli za maendeleo na
kuendeleza umoja na mshikamano miongoni mwao.






0 maoni:
Chapisha Maoni