Idadi ya mauzo ya Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) imepanda katika kipindi cha wiki iliyopita baada ya hisa kupanda kwa asilimia 49 kutoka 72,4000 hadi milioni 1.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Afisa Masoko Mwandamizi wa DSE Marry Kinabo amesema idadi ya mauzo imepanda mara mbili zaidi kutoka bilioni 3.8 hadi 9 bilioni.
“Kampuni tatu zinazoongoza kwa idadi ya hisa zilizouzwa na kununuliwa ni TBL kwa asilimia 54, SWISS 16 asilimia na CRDB asilimia 11,” amesema Kinabo.
Aidha, Kinabo amesema ukubwa wa mtaji wa soko la DSE umepanda kwa asilimia 2.48 kutoka trilioni 20.8 na kufikia trilioni 21.3.
“Pia ukubwa wa mtaji wa makampuni ya ndani umebaki kwenye kiwango kilekile cha trilioni 8.2.Viashiria katika sekta ya viwanda wiki hii imeshuka kwa alama 2.62 baada ya bei za hisa za TBL kushuka kwa asilimia 0.08,” amesema
Amesema sekta ya huduma za kibenki na kifedha wiki hii imepanda kwa alama 3.38 baada ya kupanda bei kwenye kaunta za DSE kwa asilimia 12.04.
“Sekta ya huduma za kibiashara wiki hii iko vilevile baada ya bei za hisa za Swissport kubaki tsh 3,543.02,” amesema.