Jumamosi, 10 Septemba 2016

Lindi na Mtwara kuunganishwa gridi ya taifa


 REA mtambo wa Umeme
Serikali imeanza kutatua changamoto za umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara kwa kuiunganisha mikoa hiyo kwenye umeme wa gridi ya taifa kupitia njia ya KV 400.
Akijibu swali la Mhe. Vedasto Ngombale lililohusu kiini cha ukatikaji wa umeme leo mjini Dodoma, Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo amesema kuwa suala la umeme kutoka Lindi hadi Mtwara linachangamoto nyingi za kiufundi ambapo hupelekea tatizo hilo kijitokeza.
Prof. Muhongo amesema kuwa mitambo ya Somangafungu inachangamoto kwani umeme unaofuliwa kutoka mitambo hiyo unatumika katika Wilaya za Kibiti, Kilwa na Rufiji ambapo hutumia Megawati 7.5 kwa kutumia gesi asilia.
Aidha, Serikali kupitia Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO) imeanza ukarabati katika Wilaya za Kibiti, Kilwa na Rufiji wa mitambo miwili yenye uwezo wa kuzalisha umeme kwa jumla ya Megawati 5 unaotarajiwa kukamilika Novemba, 2016 na utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 3, ambapo ufufuaji wa mtambo wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2.5 unategemewa kuanza mwezi Oktoba mwaka huu.
Kwa upande mwingine Naibu Waziri wa Nishati na Madini Medard Kalemani amesema kuwa Serikali imeanza utekelezaji wa ujenzi wa njia ya umeme itakayounganisha Wilaya ya Liwale na Nachingwea ambapo kwa sasa zinatumia umeme kutoka kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia Gesi Asilia kilichopo Mtwara.
Naibu Waziri huyo, amesema kuwa hatua iliyofikiwa kwa mpango huo ni ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa KV 33 yenye urefu wa Kilomita 14.5 kutoka Nachingwea hadi kijiji cha Luponda na kilomita 73 kutoka Liwale hadi kijiji cha Nangano kuelekea Nachingwea.
Zaidi ya hayo, TANESCO inaendelea na ukaguzi, usafirishaji na ukarabati wa miundombinu ya kusambaza umeme kwa lengo la kuwaondolea wananchi kero ya kukatika kwa umeme hatua ambayo itaondoa tatizo katika maeneo hayo.
Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, Dodom

0 maoni:

Chapisha Maoni