WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali imedhamiria kuendeleza sekta ya viwanda kama mkakati wa
kukuza uchumi ili nchi iweze kutoka kwene umaskini na kufikia uchumi wa
kati.
Waziri Mkuu amesema hayo leo
(Alhamisi, Aprili 14, 2016) alipofanya mazungumzo na Waziri wa Biashara
wa Oman, Dk. Ali Masoud Al Sunaidy ofisini kwake Magogoni jijini Dar es
Salaam.
Amesema mbali na kuimarishwa kwa
sekta ya viwanda, pia Serikali imelenga kuboresha sekta za nishati,
uchukuzi na kilimo ambazo zitawezesha Taifa kufikia malengo yake ya
kufikia uchumi wa kati.
“Sekta ya viwanda ni eneo ambalo
tunataka kuliimarisha kwa sababu litatuwezesha kuongeza thamani ya mazao
na bidhaa zinazozalishwa nchini jambo ambalo pia litakuza ajira kwa
vijana. Hivyo nawakaribisha mje kuwekeza nchini,” amesema.
Pia Waziri Mkuu amemuhakikishia
kuwa serikali ipo tayari kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wa kutoka Oman
kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali.
Kwa upande wake, Dk. Al Sunaidy
amefurahishwa na mazingira mazuri ya uwekezaji nchini na kwamba wapo
tayari kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali yakiwemo viwanda vya
usindikaji, kilimo kinachotumia teknolojia ya kisasa, na mafuta, gesi,
na ujenzi wa bandari.
Akitoa ufafanuzi, Waziri huyo
alisema: “Oman ina bandari ya Salala ambayo ni moja kati ya bandari bora
duniani yenye uwezo wa kupakua makontena 45 kwa saa. Lakini pia tunayo
bandari ya Sohar maarufu kwa bidhaa za viwandani ambayo ina uwezo wa
kupakua makontena 32 kwa saa,” amesema.
Dk. Al Sunaidy yuko nchini kwa
ziara ya kikazi ya siku tatu akiwa ameambatana na wafanyabiashara 80 wa
Oman kwa mwaliko wa Kiserikali kwa ajili ya kukuza ushirikiano wa
kiuchumi.
Naye Waziri wa Nishati na Madini,
Prof. Sospeter Muhongo amesema anatambua kuwa Oman imepiga hatua katika
teknolojia ya gesi asili ya kimiminika (LNG) hivyo ana imani Tanzania
itapata ujuzi kutoka kwao.
Amesema wafanyabiashara hao wana
fursa ya kuwekeza kweye ujenzi ujenzi wa viwanda vya mbolea katika mikoa
ya Lindi na Mtwara lakini pia wanaweza kuwekeza kwenye bandari za
Tanga, Bagamoyo, Kilwa, Lindi na Mtwara ambazo Serikali imepanga
kuboresha miundombinu yake.
0 maoni:
Chapisha Maoni