Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la
Michezo Taifa(BMT) Bw. Mohamed Kiganja wa kwanza kushoto akiongea na
waandishi wa habari hawapo pichani leo jijini Dar es salaam kuhusu
viongozi waliochaguliwa wa kamati ya muda ya mchezo wa Ngumi za kulipwa ,
kulia ni Katibu Mkuu wa kamati hiyo Bw. Yassin Ustaadh.
Katibu Mkuu mpya wa Kamati ya
Muda ya Mchezo wa Ngumi za kulipwa Bw. Yassin Ustaadh akisisitiza jambo
mbele ya waandishi wa habari hawapo pichani baada ya kukabidhiwa kamati
hiyo leo jijini Dar es salaam.
Waandishi wa habari wakimsikiliza
kwa makini Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Taifa(BMT) Bw.
Mohamed Kiganja hayupo pichani alipotambulisha viongozi waliochaguliwa
wa kamati ya muda ya mchezo wa Ngumi za kulipwa , kulia ni Katibu Mkuu
wa kamati.
………………………………………………………………………………..
Na mwandishi wetu -BMT
Baraza la Michezo Taifa(BMT) kwa
kushirikiana na wadau wa ngumi za kulipwa wameunda kamati ya muda kwa
ajili ya kuratibu na kusimamia maendeleo ya mchezo huo ndani na nje ya
Nchi.
Akizungumza na waandishi wa
habari Kaimu Katibu Mkuu wa BMT Bw. Mohamed Kiganja amesema kuwa
wameamua kuunda kamati ya muda ya mchezo huo itakayoongozwa na Katibu
Mkuu Yassin Ustaadh kutoka TPBO na Makamu katibu Mkuu Chaulembo Palasa
kutoka Chama cha Ngumi za kulipwa Tanzania(TPBC) kwa sababu hakukuwa na
chombo kimoja kinachoratibu Ngumi za kulipwa nchini.
“Tuliamua kukutana na wadau wa
mchezo wa ngumi za kulipwa mapema mwezi huu wakiwamo TPBO, TPBC,TPBC
Limited , PST na KBF ili tuweze kupata chombo kimoja imara cha
kuratibu mchezo wa ngumi za kulipwa nchini” alisema Bw. Kiganja.
Aidha Bw. Kiganja ameongeza kuwa
viongozi waliochaguliwa wafanye kazi kwa bidii na sio kuongea sana
ikiwemo kuwasilisha katiba ya kamati hiyo ndani ya siku 90 ili kuweza
kuufikisha mbali mchezo huo na kuiletea sifa na heshima Tanzania katika
mashindano ya kimataifa.
“ Natoa wito kwa viongozi wa
kamati hii wasifanye mzaha katika suala hili ikiwa kama mwanakamati
hawezi kufanya kazi aseme mapema ili achaguliwe mwengine kwa manufaa ya
Taifa” aliongeza Bw. Kiganja.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa
kamati hiyo Bw. Yassin Ustaadh amesema kuwa wapo tayari kufanya kazi na
kuufikisha mchezo huo mbali katika Nyanja za kimataifa na kuwataka
mashabiki wakae mkao wa kula.
Mbali na hayo Bw. Ustaadh
amewataka waandaaji wa mapambano hayo ambao hawana sifa na vigezo kukaa
mbali na shughuli hiyo kwani hawahitaji ubabaishaji katika tasnia hiyo
vinginevyo watatumbuliwa.
0 maoni:
Chapisha Maoni