Ijumaa, 8 Aprili 2016

VYOMBO VYA HABARI NCHINI VIMETAKIWA KUANDAA VIPINDI VYA KUELIMISHA JAMII NA KUJENGA UZALENDO

1Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye akisaini kitabu cha wageni alipowasili katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony John Mtaka (kushoto) jana wakati wa ziara yake mkoani hapo kukutana na wadau wa sekta anazozisimamia pamoja na kutoa vitendea kazi kwa maafisa habari wa mkoa huo.
6Kaimu katibu msaidizi CCM Mkoa wa Simiyu Bw. Gelison Nyamwihula akitoa taarifa ya chama mkoani simiyu kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye (katikati) alipotembelea ofisi za CCM jana mkoani humo. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony John Mtaka
2Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu Bibi. Mwamvua Jilumbi (aliyesimama) akitoa taarifa ya Mkoa wa Simiyu upande wa sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa waziri mwenye dhamana na sekta hizo Mhe. Nape Nnauye (kushoto) alipofanya ziara jana mkoani hapo kujua hali ya sekta hizo pamoja na kutoa vitendea kazi kwa maafisa habari wa mkoa huo. Wapilikushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony John Mtaka
3Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) Kanda ya ziwa Eng. Lawi Odiero (aliyesimama) akijibu hoja wakati wa ziara ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye  kukutana na wadau wa sekta anazozisimamia jana Mkoani Simiyu.
4Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye akikagua iPad kabla ya kumkabidhi afisa habari wa Mkoa wa Simiyu Bibi. Stella Kalinga (kulia) wakati wa ziara yake mkoani humo kukutana na wadau wa sekta anazozisimamia jana Mkoani Simiyu.
5 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye (kushoto) akizungumza na waandishi wa Mkoa wa Simiyu baada ya kufanya ziara yake jana mkoani humo kwa kukutana na wadau wa sekta anazozisimamia pamoja na kutoa vitendea kazi kwa maafisa habari wa mkoa huo.
Picha na: Genofeva Matemu – Maelezo, Simiyu
………………………………………………………………………………………….
Na: Genofeva Matemu – Maelezo, Simiyu
Vyombo vya habari nchini vimetakiwa kuandaa vipindi vya kuelimisha na kupunguza burudani kwa kuongeza idadi ya vipindi vya kujenga uzalendo, amani, mshikamano pamoja na umoja wa kitaifa
Rai hiyo imetolewa na Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) Kanda ya Ziwa Eng. Lawi Odieri wakati wa ziara ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye alipokutana na wadau wa sekta anazozisimamia jana Mkoani Simiyu.
“Mamlaka ya mawasiliano inafuatilia kwa karibu maudhui ya vyombo vya habari ili kuepusha maudhui potofu na hatarishi yatakayoweza kuondoa mshikamano na uzalendo tulio nao” alisema Eng. Odieri
Aidha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kutoa uwepo wa masafa ya kuanzishia vituo vya utangazaji katika Mkoa wa Simiyu pamoja na mikoa mingine ya jirani ili kuweza kuongeza idadi ya vituo vya utangazaji ambapo kwa mkoa wa Simiyu hadi sasa kuna kituo kimoja tu cha utangazaji.
Mhe. Nauye amesema kuwa uwepo wa vituo vya kutosha vya utangazaji katika mkoa wa Simiyu vitasaidia kutangaza vivutio vya utalii wa kiutamaduni vilivyopo mkoani Simiyu pamoja na kuinua wasanii wa mkoa huo kwa kuwapatia nafasi ya kurusha nyimbo zao katika vituo hivo.
Mpaka sasa idadi ya vituo vya redio nchini zenye leseni imeongezeka na kufikia vituo 123, wakati idadi ya vituo vya televisheni zenye leseni katika mfumo wa dijitali nchini umefikia 26 huku kanda ya ziwa ikiwa na jumla ya vituo vya redio 23 na kituo kimoja cha televisheni.

0 maoni:

Chapisha Maoni