PICHA NA IKULU
…………………………………………………………………………………………….
Waziri Mkuu Mstaafu wa Kenya
Mheshimiwa Raila Amolo Odinga amerejea nchini Kenya baada ya kumaliza
mapumziko yake ya siku tatu huko Lubambangwe katika Kijiji cha Mlimani,
Wilaya ya Chato Mkoani Geita, alikomtembelea Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli aliyepo mapumzikoni.
Akizungumza katika uwanja wa
michezo wa shule ya Sekondari ya Chato kabla ya kuruka kwa Helkopta,
Mheshimiwa Odinga amemshukuru rafiki yake Rais Magufuli kwa kumpokea na
pia amewashukuru wananchi wa Chato kwa ukarimu wao kwa wageni.
Mheshimiwa Odinga pia amesema ana
imani kuwa Rais Magufuli ataisaidia Tanzania kukabiliana na changamoto
mbalimbali ikiwemo umasikini unawakabili wananchi wake.
“Lakini mimi najua yeye mwenyewe
ana maono, anaona mbele na anajua yale ambayo yanatakiwa yafanyike ili
Tanzania iinuke, itoke katika hali ya ufukara na kuwa katika hali ya
maendeleo zaidi” Amesema Mheshimiwa Odinga.
Mheshimiwa Raila Amolo Odinga na
Mkewe Mama Ida Odinga waliwasili Chato tarehe 02 April, 2016 kwa
mapumziko na kuisalimia familia ya Rais Magufuli ambayo ni familia
rafiki.
Katika Hatua nyingine Rais
Magufuli ameahidi kutoa madawati na vitabu kwa wanafunzi wa shule tatu
za Msingi zilizopo Chato, ambao walijitokeza katika uwanja wa Sekondari
wa Chato, wakati Rais Magufuli akimuaga mgeni wake Waziri Mkuu Mstaafu
wa Kenya Raila Odinga.
Shule hizo ni Chato, Kalema na Kitela.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Chato
04 April, 2016






0 maoni:
Chapisha Maoni