Halmashauri ya Jiji la Tanga ipo hatarini
kuvunjwa kufuatia vurugu za madiwani wa CCM na CUF baada ya kushindwa kuelewana
katika kikao kilichositishwa leo na Mkurugenzi Mtendaji.
Kikao hicho cha baraza la madiwani wa
Halmashairi ya Jiji la Tanga kwa mujibu wa barua za mwaliko walizopewa madiwani
hao kilikuwa ni cha mwendelezo wa mkutano wa Desemba 19, mwaka jana ambacho pia
kilivunjika baada ya kutokea vurugu.
Chanzo cha kuvunjika kikao cha leo ni
baada ya diwani wa kata ya Tangasisi (CUF) ambaye pia ni Naibu Meya, Mohamed
Haniu kuchukua kipaza sauti na kutangaza kwamba kama wanataka kikao hicho
kiendelee ni lazima ufanyike uchaguzi wa Meya.
“Kwenye wito wa barua za kikao hiki
hakuna ajenda ya uchaguzi kwa hivyo tukubaliane kwanza kwamba tunaanza na
uchaguzi wa Meya ndipo tuendelee kwa sababu hatuna meya hadi sasa,”alisema
Haniu.
Tangazo hilo lilisababisha madiwani wa
kutoka chama cha wananchi (CUF) kushangilia jambo lililomlazimu Meya wa Jiji,
Mohamed Mustapha (Selebosi) kutamka kwamba kikao anakiahirisha.
Tamko la Selebosi lilisababisha madiwani
wa CUF kushangilia kwa mara ya pili huku wakiimba nyimbo za kukisifu chama
hicho.
Baada ya kuahirishwa kwa kikao hicho,
Meya wa Jiji hilo, Mohamed Selebosi, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Abdullah Lutavi,
Mbunge wa Jimbo la Tanga, Mussa Mbarouk na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Dk Wedson
Sichalwe waliingia katika ofisi ya Mkurugenzi kufanya kikao chao cha ndani.
Akizungumza na waandishi wa habari,Kaimu
Mkurugenzi , Sichalwe alisema ajenda ambazo zilikuwa zijadiliwe ni kuunda
kamati za kudumu za halmashauri, kupanga ratiba za vikao vya halmashauri,
kupokea taarifa ya utendaji wa halmashauri katika kipindi ambacho madiwani
hawakuwepo na kupokea taarifa ya Serikali.
“Kama mlivyoshuhudia kikao
kimevunjika,inapotokea vurugu kama vile hakuna sababu ya kuendelea na kikao,
sheria inamruhusu Meya kukivunja” alisema Dk Sichalwe na kusisitiza kuwa
taarifa zaidi atatoa baadaye.
Diwani wa Kata ya Duga (CUF), Halid
Rashid alisema watakuwa tayari kuendelea na kikao iwapo madiwani wa CCM watakubali
uchaguzi wa nafasi ya meya ufanyike upya kwa sababu hawamtambui Mohamed Mustafa
kama Meya.
“Ni bora Halmashauri ya jiji ivunjwe kama
Serikali inalazimisha tumtambue Selebosi kuwa ni Meya, sisi hatutakubali akae
mbele kuongoza kikao aje huku ndiyo kikao kiendelee” alisema Halid.
Mohamed Haniu (CUF) alisema anaamini Mkuu
wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela anaweza kumaliza mgogoro wa nafasi ya Meya wa
Tanga kwa kutumia busara ya kuamuru uchaguzi wa meya ufanyike upya.
Diwani wa kata ya Chumbageni (CCM) Saida
Gaddafi aliwataka madiwani kutoka chama cha CUF kukubali matokeo yaliyomtangaza
Selebosi kuwa Meya kwa sababu hata wao walimkubali Mohamed Haniu kuwa Naibu
Meya.
Mkuu wa Wilaya ya Tanga aliwahimiza
madiwani wa Jiji kukubaliana ili vikao vya kupitisha miradi ya maendeleo ya
wananchi viweze kuendelea.
Dalili za kutokea vurugu katika kikao
hicho zilijitokeza mapema kufuatia jeshi la polisi kumshikilia Mwenyekiti wa CUF
Wilaya ya Tanga na aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Meya wa jiji la Tanga, Rashid
Jumbe asubuhi kabla ya kuanza kikao hicho.
Taarifa za kushikiliwa na jeshi la Polisi
diwani huyo zilienea na hata kikao kilipoanza hakuwepo ukumbini ambapo madiwani
wenzake walisema alikamatwa kwa madai ya kuratibu shughuli za matangazo
kuhusiana na kikao hicho kwa kutumia gari lililopita mitaani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Tanga,Leonard Paul alithibitisha kukamatwa kwa diwani Rashid Jumbe na kwamba
alikuwa akituhumiwa kutangaza mitaani kwa kutumia gari kuhusu kikao hicho.






0 maoni:
Chapisha Maoni