RAIS
John Magufuli ameahirisha shamrashamra za maadhimisho ya siku ya
Muungano na hivyo kuwezesha kuokoa zaidi ya Sh bilioni mbili, alizoagiza
zikaanzishe upanuzi wa barabara inayokwenda Uwanja wa Ndege wa Mwanza.
Kwa
mujibu wa taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari kutoka Chato mkoani
Geita ambako Dk Magufuli yuko mapumzikoni nyumbani kwake, Rais
ameelekeza siku hiyo itakuwa ya mapumziko kama kawaida, na Watanzania
waiadhimishe wakiwa majumbani kwao ama katika shughuli zao binafsi.
Sherehe
za Muungano huadhimishwa kila Aprili 26 kusherehekea kuzaliwa kwa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ilianzishwa Aprili 26, 1964 baada
ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
“Kufuatia
kuahirishwa kwa shamrashamra hizo, Rais Magufuli ameelekeza kuwa fedha
zilizopangwa kutumika kwa ajili ya kugharamia vinywaji, vyakula,
gwaride, halaiki, burudani mbalimbali na hafla ya usiku ambazo ni zaidi
ya shilingi bilioni mbili, zitumike kuanzisha upanuzi wa barabara ya
“Mwanza - Airport” katika eneo linaloanzia Ghana Quaters hadi Uwanja wa
Ndege wa Mwanza,” ilieleza taarifa ya Ikulu kutoka Chato.
“Barabara
hiyo inafanyiwa upanuzi ili kukabiliana na kero ya msongamano mkubwa wa
magari ambao unaathiri shughuli za kila siku za wananchi,” ilifafanua
taarifa hiyo ya Ikulu.
Tangu
aingie madarakani, Rais Magufuli alieleza azma ya Serikali yake ya
Awamu ya Tano kubana matumizi na katika hatua alizochukua ni kufuta
safari za nje ya nchi zisizo na tija, mikutano na makongamano, pamoja na
kuahirisha sherehe mbalimbali na kuelekeza fedha zake katika masuala ya
huduma za jamii.
Aliahirisha
sherehe za Siku ya Uhuru, Desemba 9, mwaka jana na kutangaza siku hiyo
kuwa ya kufanya usafi nchi nzima ili kukabiliana na ugonjwa wa
kipindupindu katika dhana ile ya Uhuru ni Kazi.
Rais
Magufuli aliagiza fedha zilizokuwa zitumike kwa sherehe hizo, Sh
bilioni nne zikatumike kwa ajili ya upanuzi wa Barabara ya Bagamoyo
kutoka Mwenge-Morocco, Dar es Salaam yenye urefu wa kilometa 4.3.
Aidha,
Rais Magufuli alisitisha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Kitaifa, ambayo
yalikuwa yafanyike kitaifa mkoani Singida, Desemba mosi, mwaka jana.
Badala
yake, aliagiza fedha zote ambazo zilitengwa na serikali pamoja na
wahisani mbalimbali kwa ajili ya maadhimisho hayo, zielekezwe kununua
vifaa tiba na vitendanishi. Serikali ilitenga kiasi cha Sh milioni 18
kwa ajili ya maadhimisho hayo huku kila mshiriki katika maonesho hayo
akichangia kiasi cha Sh 500,000.
Awali
Rais Magufuli aliagiza fedha zilizotengwa kwa ajili ya hafla ya
uzinduzi wa Bunge zaidi ya Sh milioni 225, ziende kununulia vitanda kwa
ajili ya wagonjwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam.
Wakati
huo huo, Waziri Mkuu mstaafu wa Kenya, Raila Odinga amerejea nchini
Kenya baada ya kumaliza mapumziko yake ya siku tatu Lubambangwe katika
Kijiji cha Mlimani, Wilaya ya Chato mkoani Geita alikomtembelea Rais
Magufuli aliyepo mapumzikoni.
Akizungumza
kwenye Uwanja wa Michezo wa Shule ya Sekondari ya Chato kabla ya kuruka
kwa helikopta, Raila alimshukuru rafiki yake Rais Magufuli kwa kumpokea
na pia aliwashukuru wananchi wa Chato kwa ukarimu wao kwa wageni.
Pia
alisema ana imani kuwa Rais Magufuli ataisaidia Tanzania kukabiliana na
changamoto mbalimbali, ikiwemo umasikini unaowakabili wananchi wake.
“Lakini mimi najua yeye mwenyewe ana maono, anaona mbele na anajua yale
ambayo yanatakiwa yafanyike ili Tanzania iinuke, itoke katika hali ya
ufukara na kuwa katika hali ya maendeleo zaidi,” alisema Raila.
Raila
na mkewe, Mama Ida Odinga waliwasili Chato, Jumamosi iliyopita kwa
mapumziko na kuisalimia familia ya Rais Magufuli ambayo ni familia
rafiki.
Katika
hatua nyingine, Rais Magufuli ameahidi kutoa madawati na vitabu kwa
wanafunzi wa shule tatu za msingi zilizopo Chato, ambao walijitokeza
Uwanja wa Sekondari wa Chato wakati Rais Magufuli akimuaga mgeni wake
Waziri Mkuu mstaafu wa Kenya, Raila Odinga.
|
0 maoni:
Chapisha Maoni