MAGARI
zaidi ya 1,500 jana yalikwama kwa saa tisa katika eneo la Chalinze
Nyama ,Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma na kusababisha adha kubwa kwa
abiria waliokuwa wakisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Kanda ya Ziwa na
wale wa kutoka Dodoma kwenda Morogoro na Dar es Salaam.
Kulikuwa
na msongamano mkubwa wa magari zaidi ya kilometa 10 kutoka upande mmoja
kwenda upande mwingine kutokana na mafuriko hayo yalisababishwa na mvua
iliyonyesha kuanzia juzi jioni na kusababisha barabara kujaa maji kiasi
cha njia kushindwa kuonekana.
Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana ambaye alifika eneo la Chalinze
Nyama kujionea hali halisi, aliwataka madereva kuchukua hadhari ya hali
ya juu pindi wanapopita kwenye eneo lililojaa maji. Pia aliwataka
wananchi wanaoishi mabondeni kuhama kwani mvua bado zipo na zinaendelea
kunyesha.
Mvua
hiyo iliyonyesha usiku kucha, ilianza saa tatu usiku hadi asubuhi,
imeharibu pia miundombinu ya barabara kwani nguzo za umeme katika maeneo
kadha wa kadha pembezoni mwa barabara kuu katika Wilaya ya Chamwino
eneo la Kijiji cha Chalinze Nyama zilionekana kuinama na kukaribia
kuanguka.
Kulingana
na maelezo ya wakazi wa kijiji hicho ambako magari yote yaliyoanza
safari ya kutoka mjini Dodoma kwenda Dar es Salaam na Morogoro yalikwama
baada ya maji mengi kusambaa juu ya daraja na kusababisha magari
yashindwe kupita, walisema yalisababisha hofu kubwa kwa wenyeji na
wasafiri pia.
Maji
ya mafuriko hayo yaliyokuwa yakitiririka kutoka maeneo ya milimani Kata
ya Hombolo yalianza kujaa barabarani na maeneo ya kuzunguka nyumba za
wakazi wa Kijiji cha Chalinze Nyama, yakiwafanya wenyeji kukaa nje
maeneo ya mwinuko wakiwamo akina mama na watoto wao wadogo pamoja na
wazee.
Takribani
kaya zisizopungua 100 na magari zaidi ya 1,500 yakiwamo mabasi ya
abiria na malori yalizuiwa kuendelea na safari zao na askari wa usalama
barabarani ili kuepusha kutokea kwa ajali au kusombwa na maji. Kwa kiasi
barabara hiyo kuu ilifungwa kwa muda kuanzia saa 12:00 alfajiri hadi
saa tisa alasiri baada ya maji kupungua ndipo yaliporuhusiwa kuendelea
na safari.
“Ilipofika
saa nne hivi kuna basi lilijaribu kupita lakini likaserereka abiria
wakatokea madirishani baada ya hapo hakuna gari ambalo liliruhusiwa
kupita mpaka sasa,” alisema mkazi mmoja wa Chalinze Nyama.
Aidha,
familia inayosadikiwa ni ya Shehe wa Msikiti wa Jumuiya ya Ahmaddiyya
uliopo kijijini hapo jirani na barabara itokayo Dodoma kwenda Dar es
Salaam, walijikuta nyumba yao imezungukwa na maji ya mafuriko hayo na
kushindwa kutoka nje hadi Jeshi la Zimamoto kutoka Dodoma Mjini
walipokuja kuwanusuru.
Familia
hiyo ya mama na wanawe wanne wadogo, ilijikuta katika wakati mgumu, na
mama huyo alisema hadi alfajiri hawakujua endapo maji yalizunguka nyumba
yake na kusababisha hofu na wao kushindwa kutoka nje.
Pia
mvua hiyo imesababisha miundombinu ya umeme hususani nguzo
zinazosambaza umeme kwenye kijiji hicho kwenda hadi wilayani Kongwa
kuanguka na kusababisha umeme kukatika tangu usiku huo wa saa tisa usiku
hadi jana. Mafundi wa Tanesco walionekana wakifanya kila juhudi
kurekebisha hali hiyo ili zisianguke katika maeneo ya watu.
Pia
nyumba za wanakijiji wapatao 30 wa Kijiji cha Nzali, Kata ya Hombolo
Wilaya ya Chamwino pia hawana mahali pa kuishi kutokana na athari za
mvua hiyo. Hadi saa tisa alasiri, maji yalikuwa yakitiririka kwa wingi
japo magari yalishaanza kuruhusiwa kuendelea na safari.
Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Farida Mgomi alisema serikali itahakikisha wananchi walioathirika wanapata huduma zote.
|
0 maoni:
Chapisha Maoni