Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limetoa nje vifaa vya ofisi ya gazeti la Tanzania Daima linalomilikiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ,Freeman Mbowe, kwa madai kuwa ameshindwa kulipa deni analodaiwa kwa muda mrefu na kwamba vifaa vyake vitarudishwa katika ofisi hiyo endapo atalipa deni analodaiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika zoezi hilo la utoaji vifaa linaloendelea hadi sasa, Meneja Kitengo cha Ukusanyaji Madeni NHC, Japhet James Mwanasenga amesema Mbowe anadaiwa Bilioni 1 na milioni 117 hadi mwezi Agosti mwaka huu, na kudai kuwa sheria zote zilifuatwa ambapo mdaiwa alipewa barua ya notisi na ya dalali.
Mwanasenga aliongeza kuwa, “Mdaiwa alipewa muda wa siku 30 kulipa deni, lakini hakulipa ndipo NHC ilipompa muda mwingine tena wa siku 14 ambao pia hakulipa.” Ofisi hizo zipo mtaa wa Mkwepu maeneo ya Posta jijini Dar es Salaam.
“Mdaiwa alipewa notisi za kawaida na sisi tunafuata, sheria ya nyumba ni sheria ya nchi alipewa siku 30 hakulipa, alipewa Siku 14 tena hakulipa, sasa hatuna namna yoyote zaidi ya kumuondoa kwenye nyumba, hili deni ni la miaka mingi mkija ofisini nitawaambia lilianza muda gani, ” amesema
Ameongeza kuwa ” Nadhani hilo la vyombo kupigwa mnada ni suala la dalali, Shirika hili ni shirika mama mpaka tumefikia hatua hii kuna taratibu zimefuatwa na ni lazima mteja asikilizwe hivyo ameshasikilizwa na kutoa maelezo yake, “
Amesema Mbowe hakuwa na ubia wowote na shirika hilo na kudai kuwa ni mpangaji wa kawaida kama walivyo wengine.
“Zoezi linaloendelea wakati huu ni endelevu tutawapitia wapangaji wote wadaiwa ili kuhakikisha serikali inapata mapato yake, amepewa notisi zote hadi za dalali na anafahamu hilo, anadaiwa kodi hadi ya mwezi August,2016,
“Wapangaji walipe kodi kuepusha usumbufu ukikatiwa maji utachota kwa jirani ukifukuzwa huwezi kwenda na familia yako kwa jirani, ” alisema.
Kwa upande wa Dalali kutoka kampuni ya Fosters Auctioneers iliyopewa tenda ya kutoa vifaa hivyo, Joshua Mwaituka amesema mali zote zilizotolewa katika ofisi hiyo zitakuwa chini ya kampuni yake hadi pale atakapolipa na pia amesema alitoa notisi ya siku 14 iliyoisha jana.
9a54b2e2-6d35-4709-838e-1ce1360d0e05
45d2dda4-c114-483c-8e3a-4615dbd21344
04911a7e-6d68-4974-a25a-0cb6ff8f82d3
5959ec4f-edc6-4786-b163-8db5aea1d80d
1199079c-beab-4989-8d55-1109d42ef924
ff6c2d4d-86bf-49b4-9159-9c8d5b65ea7c
ff4897bd-293d-45c3-b656-cd7849ea11fa