Fujo zimezuka katika mji mkuu wa Gabon, Libreville baada ya Rais Ali Bongo Ondimba kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Jumamosi nchini humo.
Mgombea wa upinzani Bwana Jean Ping amesema watu wawili wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa baada ya vikosi vya usalama kuvamia makao makuu ya chama chake cha UFC na kufanya mashambulizi.
“Walishambulia mwendo wa saa saba za usiku,ni kikosi cha wanajeshi na walinzi wa rais. Walikuwa wanarusha mabomu kutoka kwenye helikopta na kisha baadaye wakashambulia kutoka ardhini,” amesema Ping
Bw Ping, ambaye hakuwa katika makao makuu hayo wakati  wa mashambulizi hayo ameomba msaada wa kimataifa ili kuwalinda raia wa nchini humo kutokana na ghasia na fujo zinazoendelea.
Bw Ping amepinga matokeo ya urais ambayo yameonyesha Rais Bongo ameshinda kwa asilimia 49.8% ya kura huku yeye  akifuatia kwa asilimia 48.2% ya kura hizo  huku kura zilizowatenganisha zikiwa ni kura 5,594 tu.
Bw Ping amesema kuwa uchaguzi huo ulijaa udanganyifu na hakuna ajuaye hasa nani alishinda, ila ametaka takwimu za ushindi kutoka kila kituo zitolewe ili haki iweze tendeka.
Waandamanaji wameingia barabarani muda mfupi baada ya matokeo ya uchaguzi huo kutangazwa huku wakichoma moto majengo ya bunge na kukabiliana na polisi wa kutuliza ghasia na  fujo nchini humo
Serikali ya nchini Gabon  imesema kuwa inawatafuta wahalifu wenye silaha ambao wanadhaniwa kuhusika na kuchoma moto majengo ya bunge nchini humo.
Na Hashim Ibrahim (UDSM-SJMC)