Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa
(NIDA) itaanza kutoa Vitambulisho vipya vya Taifa vyenye saini kwa
wananchi wote waliokamilisha taratibu za usajili na utambuzi na
kuchukuliwa alama za kibaiolojia (Alama za vidole, Picha, Saini ya
Kielektroniki).
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi
Mkuu wa NIDA Bw. Andrew Massawe; utekelezaji wa zoezi hilo utaanza rasmi
Jumanne tarehe 14 Septemba 2016 katika ofisi zote za NIDA zikiwemo
ofisi za Wilaya zilizoanza usajili Tanzania Zanzibar na mikoa ya
Dar-es-salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Morogoro, Tanga, Arusha,
Kilimanjaro, na Ruvuma) pamoja na waheshimiwa Wabunge Dodoma.
Waombaji wote ambao Vitambulisho
vyao viko tayari watatumiwa ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) katika simu
zao za kiganjani (mkononi) kufahamishwa kufika katika vituo vya Usajili
kuchukua Vitambulisho vyao.
Kuhusu wananchi ambao
tayari wana Vitambulisho visivyo na saini; Bw. Massawe amesema…. “
Mamlaka inakusudia kubadilisha vitambulisho vyote vya zamani visivyo na
saini, ila kwa sasa vitambulisho vya zamani vitaendelea kutumika
sambamba na vipya wakati taratibu za kuendelea kuvibadilisha
zikiendelea” alisisitiza.
Amesema kutokana na uwepo
wa njia nyingi na salama za kusoma taarifa za mwombaji zilizomo ndani ya
kifaa maalumu kilichofichwa kwenye kadi ya mtumiaji (chip); ndiyo maana
vitambulisho vya zamani vitaendelea kutumika katika huduma mbalimbali
zinazohitaji kumtambua mtumiaji kabla ya kupata huduma.
Akizungumzia wananchi ambao
hawakuwahi kusajiliwa, Bw. Massawe amesisitiza kwamba wananchi wote
ambao hawakuwahi kusajiliwa na wana umri wa miaka 18 na kuendelea; kwa
mikoa ambayo tayari kuna ofisi za usajili, kuendelea kujitokeza kwa
wingi kusajiliwa ili kupata Vitambulisho vya Taifa kwani zoezi la
usajili ni endelevu.
“ Kwa wale wananchi ambao
walisajiliwa kupitia Daftari la Mpiga kura NEC; NIDA iko mbioni kuanza
kutoa nambari za utambulisho wakati tukiendelea kukamilisha taratibu za
usajili ili kupata utambulisho kamili na kuanza kunufaika na matumizi
mapana ya Utambulisho wa Taifa wakati taratibu za uzalishaji wa
Vitambulisho zikiendelea”.
Wananchi wanakumbushwa kutunza
vizuri Vitambulisho vyao ili kuepuka gharama kwani kitambulisho cha
Taifa kwa mara ya kwanza kitatolewa bure na iwapo kitapotea, ili kupata
kingine lazima mtumiaji akilipie.
Kwa sasa vitambulisho vya Taifa
vimeanza kutumika katika baadhi ya huduma nchini hususani kwenye mabenki
kwa ajili ya kufungua akaunti na kuthibitisha taarifa za mtu kabla ya
kupatiwa huduma. Taratibu za kupanua wigo wa matumizi ya Vitambulisho
kielektroniki kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali zinaendelea.
0 maoni:
Chapisha Maoni