.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. George
Simbachawene (kulia) akiongea na Mama Graca Machel (kushoto)
alipomtembelea ofisini kwake leo jijini Dar es salaam.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. George Simbachawene (kulia) akiagana na Mama
Graca Machel (kushoto) mara baada ya mazungumzo ofisini kwake leo jijini
Dar es salaam.
(Picha na Eleuteri Mangi-MAELEZO)
……………………………………………………………………
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
Watoto wa kike 20,000 kutoka mkoa wa Mara watanufaika kwa
fursa ya kupata elimu kupitia Mfuko wa Graca Machel (Graca Machel Trust)
ambao umejikita katika kusaidia wanawake na watoto nchi kadhaa za
Afrika.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. George
Simbachawene mara baada ya mazungumzo na Mama Graca Machel
alipomtembelea ofisini kwake leo jijini Dar es
salaam.
“Ni fursa nzuri ya
kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi kuwasaidia watoto wetu wa
kike kielimu ambayo itawasaidia kutoka katika jamii ya umasikini na
kuhakikisha wamepata fursa ya kuvuka umri wa vishawishi na maamuzi
yasiyo sahihi” alisema Waziri Simbachawene.
Watoto hao watakaonufaika na
Mfuko huo mkoani Mara watatoka katika shule 104 ambapo inatarajiwa
kuwafikia watoto wa kike wengi zaidi mara baada kuanza kutoa huduma hiyo
mkoani humo.
Waziri Simbachawene amesema
kuwa Mama Graca Machel amechagua kuja katika Tanzania kutokana
ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Msumbiji kwa kuzingatia
mchango mkubwa wa Tanzania kwa nchi hiyo.
\
Aidha, Waziri Simbachawene
amemshukuru Mama Graca Machel kwa kujali na kuuchagua mkoa wa Mara ambao
ndio mkoa alipozaliwa Mwasisi wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere.
Kwa upande wake Mama Graca
Machel amemshukuru Waziri Simbachawene kwa mapokezi na ushirikiano
alioupata katika Serikali ya Awamu Tano iliyopo madarakani na kuahidi
kuendelea kusirikiana nao ambapo anaamini mpango wa kuwasaidia watoto wa
kike kupita taasisi yake utapanuka na hatimaye kuweza kuwafikia watoto
wa kike wengi zaidi kupitia mikoa yote nchini.
“Lengo ni kuwabakisha watoto wa
kike shuleni ili wapate elimu, ni lazima tusaidiane wote, tuna kila
sababu ya kusaidiana” alisema Mama Graca Machel.
Uhusiano wa Tanzania na
Msumbiji ni wa kihistoria kwani wananchi wa nchi hizo walishirikiana
katika shughuli mbalimbali chini ya mwavuli wa unasaba na ushirikiano
katika biashara na tamaduni kwenye miji ya Unguja, Kilwa, Lindi na
Mtwara kwa upande wa Tanzania na katika miji ya Chilimbo, Tete, Pemba na
Sofala nchini Msumbiji.






0 maoni:
Chapisha Maoni